TAZARA SASA KUSUKWA UPYA KIMFUMO NA UTENDAJISerikali ya Tanzania na Zambia zimekubali kulisuka upya Shirika la Reli la nchi hizo (Tazara), kwa kufanya marekebisho ya kimfumo na kiutendaji ili kutatua matatizo ya kimuundo na kimenejimenti yanayochangia kuzorota kwa ufanisi wa shirikia hilo.

Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari, aliyoitoa juzi usiku, Rais Kikwete alisema hatua hiyo inatokana na mafanikio ya ziara yake ya siku mbili aliyoifanya nchini Zambia mwezi uliopita, kwa mwaliko wa Rais mpya wa wa nchi hiyo Egdar Lungu.
Akizungumzia usukwaji wa Tazara, Rais Kikwete alisema wamekubaliana  kuchukua hatua thabiti kutatua matatizo ya kiungozi, kifedha na kiufundi yanayolikabili shirika hilo kwa sasa.
 “Tumeelewana, hatuna budi kufanya marekebisho ya kimfumo, kiutendaji ili kutatua matatizo ya kimuundo na kimenejimenti yanayochangia kuzorota kwa ufanisi wa shirika hili”, alisema Rais Kikwete.
Katika hotuba yake hiyo alisisitiza kuwa katika mazungumzo yao na Rais wa Zambia, wameafikiana masuala yote na kukubaliana serikali za nchi hizo kutekeleza wajibu wake kwa Tazara.
 “Tumekubaliana kila nchi itekeleze wajibu wake ipasavyo kwa Tazara, michango ya fedha itolewe tufufue shirika hili muhimu kwa uchumi wa nchi zetu mbili”, alisema Rais Kikwete. 
Aidha, alisema wamekubaliana kuangalia uwezekano wa kuruhusu makampuni au mashirika mengine ya reli kutumia reli hiyo kusafirisha mizigo yao kwa kulipia ushuru wa huduma kwa shirika hilo.
 “Wazo la kuruhusu kampuni au mashirika ya reli mengine kutumia reli yetu ni wazo jema, tumeagiza Baraza la Mawaziri kulifanyia kazi wazo hili mapema iwezekanavyo”, alisisitiza Rais Kikwete.
Akizungumzia sekta ya Nishati, Rais alisema wamekubaliana nchi hizo kuendelea kushirikiana na kuimarisha bomba la mafuta la TAZAMA, ambapo pia Zambia imeelezea dhamira yake ya kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Dar es Salaam hadi Zambia.
 ‘Wameomba tukubali kuwauzia gesi asilia, nimewaambia ni jambo linalowezekana, tumekubaliana nchi zetu zilifanyie kazi ombi hilo”, alisema Rais Kikwete.
 Pamoja na ombi hilo, serikali ya Zambia imeahidi kuimarisha njia ya umeme kutoka Kasama hadi Mbala, Zambia inakoanzia njia inayoleta umeme Sumbawanga. 
Ikiwa ahadi hiyo itakamilika Rais alisema  itaondoa matatizo ya sasa ambapo umeme unaofika Sumbawanga kutoka Mbala, ni  mdogo na hauna nguvu ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani, ofisini na viwandani.
Kuhusu kuboresha huduma kwa abiria na mizigo katika mpaka wa Tanzania na Zambia eneo la Tunduma, Rais alisema wamekubaliana Tanzania ikamilishe ujenzi wa jengo litakalowezesha huduma zote muhimu za mpakani kutolewa katika jengo hilo.
Na kwamba wakati jengo hilo likisubiriwa ujenzi wake, watatumia jengo la muda kurahisisha taratibu za usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo katika mpaka wa Tanzania na  Zambia. 
Pia uboreshaji wa taratibu za forodha kwa mizigo itokayo Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kupitia Zambia unaendelea. 

No comments: