TANESCO YAKIRI ‘MADUDU’ KATIKA MFUMO WA KUUZA LUKU



Shirika la Ugavi na Usambazaji wa Umeme nchini (TANESCO), limekiri kuwepo na matatizo ya mfumo wa kununua Luku, ulioanza Ijumaa jioni wiki iliyopita  hadi jana na kuwa matatizo hayo yanatokana na mfumo wa kuuza umeme wa Luku.

Akizungumza na mwandishi jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Adrian Shogholo alisema ni kweli kuwa tatizo hilo lipo na limetokana na mfumo wa manunuzi wa umeme wa Luku.
“Ni kweli tunaomba radhi wateja wetu kwamba kuanzia Ijumaa jioni kulianza tatizo la kununua umeme wa luku, kwa wateja wetu, ila tumegundua tatizo na mafundi wetu kwa kushirikiana wa mafundi kutoka Afrika Kusini, ambao walitengeneza mfumo huo, wanalishughulikia tatizo hilo”, alisema Shogholo.
Aidha aliahidi kwamba muda wowote kuanzia leo, huduma zitaanza kupatikana na kwamba wakati tatizo hilo likiendelea kushughulikiwa, wateja wa Luku wanaweza kununua umeme kupitia benki ya CRDB, NMB na Max Malipo.
 “Kuna wateja wanaotumia simu kununua umeme, wapo waliotuma fedha na hawajarudishiwa majibu ya umeme, na wengine wamepata umeme ila wakiingiza kwenye Luku hauingii, wasihofu fedha zao ziko salama na watapata umeme, tutawatumia namba nyingine ambazo wakiingiza zitakubali”, alisema Shogholo.

No comments: