Akiwa katika maadhimisho ya kuanza mwaka wa
pili wa utume wake katika kuongoza Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu
Francis, ametoa kauli kuashiria kuwa huenda asidumu katika wadhifa huo kwa muda
mrefu ujao.
Alisema hayo juzi katika mahojiano ya ana kwa
ana na kituo kimoja cha televisheni cha
Mexico, Televisa News, baada ya kutangaza kuwa Desemba mwaka huu, Kanisa
Katoliki litaadhimisha Mwaka Mtakatifu.
Mwaka huo Mtakatifu utaanzia Desemba 8, mwaka
huu na kuisha Novemba 20, mwakani.
Inaelezwa kuwa kuzinduliwa kwa Mwaka Mtakatifu
au Jubilee, kunaendana na maadhimisho ya 50 ya kufungwa kwa Baraza la Pili la
Vatican, ambalo hukusanya maaskofu ambao huzungumzia mambo ya baadae ya kanisa.
Mwaka huo Mtakatifu utakuwa wa 29 tangu
utaratibu huo ulivyoanza mwaka 1300. Kwa kawaida Mwaka Mtakatifu huadhimishwa
kila baada ya miaka 25.
Katika tamko hilo, Baba Mtakatifu Francis
mwenye umri wa miaka 78, ameweka wazi kuwa hataadhimisha miaka mingine
mitakatifu katika siku zijazo.
“Nina
hisia kwamba utume wangu utakuwa wa muda mfupi, kama miaka minne au mitano;
sijui inaweza hata kuwa miwili au mitatu lakini miaka miwili imeshapita,”
alitabiri katika mahojiano hayo.
Hata hivyo, hakutaka kuweka wazi kama atafuata
nyayo za mtangulizi wake, Baba Mtakatifu mstaafu Benedict XVI, ambaye ameweka
historia ya kuwa Baba Mtakatifu wa kwanza kustaafu katika miaka 600 iliyopita,
baada ya kuchukua hatua hiyo mwaka 2013.
Alipoulizwa swali mahususi kama atafuata nyazo
za Baba Mtakatifu mstaafu, Benedict XVI, alijibu; “Huenda Benedict XVI akabakia
kuwa Baba Mtakatifu mstaafu pekee kwa miaka mingi ijayo, na huenda akapata
mwenzake,” na kuongeza kuwa Baba Mtakatifu mstaafu “ameonesha njia.”
Hii si mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu
Francis kuzungumzia ukomo wake, kwa kuwa amewahi kusema kustaafu kwa Baba
Mtakatifu Benedict XVI mwaka 2013, kusichukuliwe kuwa tukio la pekee.
Pia, alisema hakuchukia kuteuliwa kuwa Baba
Mtakatifu, lakini aliweka wazi kwamba katika wadhifa huo, amejikuta akipoteza
uhuru wake.
“Natamani tena kuwa na uwezo wa kutoka nje
siku moja bila mtu yeyote kunifuatilia na kunitambua nikajinunulie mahitaji
yangu,” alisema na kutabasamu.
Lengo la mahojiano hayo na kituo hicho cha
Televisa News, lilikuwa kujadili maisha yake ikiwemo mawasiliano yake na baadhi
ya watu, ambao wamekuwa wakimwandikia barua kumshirikisha katika huzuni zao na
kupata ushauri wake.
Baba Mtakatifu pia alizungumzia hali ya
uhamiaji duniani na kuibuka kwa wimbi la wakimbizi wanaokimbia umasikini, njaa
na vita katika nchi zao za kuzaliwa.
Katika mahojiano hayo yaliyochapishwa katika
kurasa 17, Baba Mtakatifu Francis alisema kwa kuwa yeye ni Baba Mtakatifu wa
kwanza kutoka Bara la Amerika ya Kusini, analazimika kuzungumzia wahamiaji na
watu masikini kwa sababu babu zake walihama kutoka Italia kwenda Argentina
kutafuta kazi.
“Watu wamekuwa wengi bila kazi, kiasi cha
kulazimika kutafuta kazi mahali pengine,” alisema Baba Mtakatifu Francis,
ambaye safari yake ya kwanza baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo,
alitembelea kisiwa cha Lampedusa, Italia
kutoa heshima kwa maelfu ya wahamiaji waliokufa wakijaribu kwenda katika Bara
la Ulaya.
No comments:
Post a Comment