MWINGEREZA ANAYEDAIWA KUUA MKE AREJESHWA KWAO


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru raia kutoka nchini Marekani, Sammy Almahri aliyekuwa anakabiliwa na mashitaka ya kumuua mke wake, ametakiwa kupelekwa nchini Uingereza na kushitakiwa katika sehemu ambayo alifanya mauaji hayo.

Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema alitoa amri hiyo baada ya kukubali ombi la upande wa Jamhuri lililowasilishwa baada ya kufuta mashitaka dhidi ya mshitakiwa huyo wiki iliyopita.
Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani wiki iliyopita na kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda, hata hivyo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliwasilisha hati mahakamani kuwa hana nia ya kuendelea kumshitaki.
Hata hivyo, baada ya kuachiwa huru, Almahri aliendelea kuwa mahabusu chini ya ulinzi hadi upande wa Jamhuri ulipowasilisha ombi la kumpeleka nchini Uingereza akashitakiwe sehemu anayodaiwa kufanya mauaji.
Almahri anadaiwa Desemba 31, mwaka 2014 nchini Uingereza ndani ya Hoteli ya Curdiff South Wiles iliyopo nchini humo, kwa makusudi alimuua mpenzi wake, Nadine Aburas.
Awali mbele ya Hakimu Lema, mshitakiwa alisomewa maelezo ya ombi hilo na kupitia Wakili wake, Mabere Marando alidai hana pingamizi kwa kuwa ndiyo matakwa ya serikali kumpeleka huko.
Mahakama iliamuru pia vitu vya mshitakiwa vilivyochukuliwa Polisi wakati alipokamatwa,  vipelekwe Uingereza na atakwenda kukabidhiwa huko.
Awali mshitakiwa huyo alipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza, alidai alipokonywa baadhi ya nyaraka zake muhimu, ana matatizo ya kiafya pia amefungiwa akaunti zake za benki.
Aliomba Mahakama itoe ruhusa ya kufunguliwa kwa akaunti hiyo pamoja na kurudishiwa nyaraka ili isiathiri familia yake kwa kuwa ana watoto wawili ambao ni wanafunzi nchini Marekani, pia ana matatizo ya kiafya, hivyo anatakiwa kuwa chini ya uangalizi wa daktari maalumu.

No comments: