MAJINA YA ABIRIA WOTE AJALI YA BASI LILILOUA 42 MAFINGA HAYA HAPA


"Ni ajali ambayo haijawahi kutokea katika maeneo haya," ni baadhi ya maneno yaliyosikika kutoka kwa wakazi wengi wa mjini Mafinga na vitongoji vyake, ambao jana walishuhudia ajali  katika historia ya mji huo.

Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania namba T 689 APJ, mali ya Cipex Company lililokuwa likiendeshwa na Maka Sebastian (26)  na basi aina ya Scania namba T438 CED, mali ya kampuni ya Majinja lililokuwa likiendeshwa na Baraka Gabriel (38).
Wakati lori lilikuwa likielekea Barabara ya Mafinga-Mbeya, basi hilo lilikuwa likitokea Mbeya kuelekea jijini Dar es Salaam.
Ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu 42 wakiwemo 40 waliokuwemo katika basi na wawili katika lori hilo, ilitokea katika eneo la Changarawe takribani kilometa 5 kutoka mjini Mafinga, mkoani Iringa, katika barabara kuu ya Mafinga-Mbeya.
Kati ya waliokufa yupo dereva wa basi hilo, huku dereva wa lori akijeruhiwa vibaya baada ya kuchomwa na kitu kama nondo shingoni mwake.
Akizungumza katika eneo la tukio, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema watu wengine 22 wamejeruhiwa vibaya na wamekimbizwa katika hospitali ya wilaya ya Mufindi, mjini Mafinga na hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa, mjini Iringa wanakoendelea kupata matibabu.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Boaz Mnenegwa alisema walilazimika kuwahamishia majeruhi 15 kati ya 22 katika hospitali ya mkoa wa Iringa baada ya hali zao kuonekana ni mbaya zaidi.
“Pamoja na kuvunjika sehemu mbalimbali za miili yao, wengi wao wameumia vichwani hali iliyotulazimu tuwakimbize katika hospitali ya mkoa wa Iringa ili wakapate huduma kwa ufanisi zaidi,” alisema.
Akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Salim Asas na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, Mungi alisema ajali hiyo ilitokea jana asubuhi saa tatu na nusu.
Kamanda Mungi alisema jeshi lake kwa kushirikiana na hospitali za Mafinga na Mkoa wa Iringa wanaendelea kutambua majina ya watu waliokufa na  majeruhi.
Kamanda Mungi alisema taarifa zao za awali zinaonesha chanzo cha ajali hiyo ni ubovu wa barabara; huku baadhi ya majeruhi wakisema dereva wa basi hilo ambaye pia alikufa papo hapo, alikuwa kwenye mwendo kasi na hata hakuwa makini kuzingatia ishara za hatari.
Mungi alisema lori na basi hilo yaligongana uso kwa uso wakati madereva wake wakishindana kuwahi kuchepuka moja kati ya mashimo makubwa yaliyopo pembezoni na katikati mwa barabara hiyo katika eneo hilo.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Jackson Manga alisema kama dereva wa basi hilo angezingatia ishara za taa kali alizokuwa akiwashiwa na dereva wa lori hilo,  ajali hiyo isingetokea.
Manga alisema katika eneo hilo lenye mteremko wa wastani, lori lilikuwa likipandisha na basi lilikuwa likishuka.
Alisema ukaidi wa dereva wa basi ulisababisha dereva wa lori aingie katika shimo kubwa katika eneo hilo, hali iliyosababisha ashindwe kulimudu gari hilo kabla ya kuvaana uso kwa uso na basi hilo.
“Baada ya kuvaana, kontena la futi 40 lililokuwa limepakiwa katika lori hilo liliruka juu kwa kishindo kikubwa, kubamiza na kufunika basi hilo,” alisema.
Mmoja wa majeruhi wa basi hilo, Kevin Humphrey ambaye kalazwa katika hospitali ya wilaya ya Mufindi alisema; “tulisikia mshindo mkubwa baada ya basi letu kugongana na lori hilo na mshindo huo ulisababishwa na kontena iliyotoka kwenye lori hilo na kupiga juu ya basi letu.”
Mwandishi alishuhudia mabaki ya basi hilo ambalo sura yake imebadilika kiasi cha kutotambulika kutokana na kuvunjwavunjwa na kontena hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema; “ajali hii ni mbaya yawezekana kuliko zote kuwahi kutokea mkoani kwetu. Ni ajali inayotuacha na majonzi makubwa.”
Kwa sababu ya uwezo mdogo wa hospitali ya wilaya ya Mufindi, Mkuu wa Mkoa huyo aliagiza miili 32 ambayo haijatambuliwa na ndugu zao ihamishiwe chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.
Uhamishaji wa miili hiyo ulifanywa na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Mufindi kwa kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mafinga.
Baadhi ya watu waliotajwa kuwepo katika basi na lori hilo ambao hata hivyo hawakuweza kufahamika mara moja, nani kafa na nani kajeruhiwa ni pamoja na Ester Emanuel, Lusekelo Enock, Jeremia Watson, Digna Solomoni na Frank Chiwango.
Wengine ni Luteni Sanga, Teresia Kamingage, Dotto Katuga, Ester Fidelis, Paulina Justine, Mbamba Ipyana, Catherine, Mwajengo, Zera Kasambala, Rebeka Kasambala, Shadrack Msigwa, Mathias Justine, Juliana Bukuku, Cristina Lyimo, Martin Haule na Dominick Mashauri.
Wengine ni Ester Willy, Lucy Mtenga, Erick Shitindi, Edwiga Kamiyeye, Frank Mbaula, Mustapher Ramadhani, Kelvin Odubi, Upendo William, Charles Lusenge, Neto Sanga, Pili Vicent, Daniel, Jacob Doketa Iman Mahenge na Juma Sindu.
Wengine waliokuwepo katika ajali hiyo wametambuliwa kwa jina moja Amadi, Musa, Elias, Raphael, Hussein na Oswald.
Habari kutoka Mbeya zinaeleza kuwa wakati basi hilo linaondoka kituoni abiria waliokuwepo kwenye basi hilo walikuwa ni 37 ambao ni: 
Baraka Ndone  ambaye ni dereva, Yahya  Hassan ambaye ni kondakta, Esther    Emmanuel, Henry Lugano, Lusekelo Enock, Jeremia  Watson, Hamad, Olga Solomon, Neto, Theresia Kaminyoge, Frank Chiwanga, Luteni Sanga, Alfred Sanga, Doto Katunga,  Juliana Bukuku, Esther Fidel,  Paulina Josia.
Wengine ni Iman Mahenge,  Catherine Mwate, Mathias Justine,  Rebeka Kasambala,  Upendo William, Mbamba Ipyana,  Ndulile Kasambala, Dk A. Shitindi, Six Erick, Frank Mbaule, Mustafa Ramadhani,  Musa, Omega Mwakasege, Shadra Msigwa, Lucy Mtanga, Charles Mweisonga, Martin Haule, Dominick Mashauri, Kelvin Ebadi, Juma Saidi,  na Nicko.
Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kutokana na ajali  iliyotokea eneo la Changarawe, Mafinga na kupoteza uhai wa watu zaidi ya 40 waliokuwa wakisafiri kwa basi hilo na wengine kadhaa kujeruhiwa.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za vifo vya watu zaidi ya 40 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika ajali hii mbaya ambayo imesababisha simanzi na majonzi makubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu,” alisema.
Aliongeza: “Huu ni msiba mkubwa na Taifa limepata pigo, hivyo naomba upokee salamu zangu za rambirambi za dhati za moyo wangu. Kupitia kwako naomba rambirambi zangu na pole ziwafikie watu wote waliopotelewa ghafla na wapendwa wao.  Namuomba Mungu azipokee na kuzilaza roho za marehemu wote mahala pema peponi, amina.”
Kikwete amewahakikishia wafiwa wote kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba wa ndugu na jamaa zao, na kuwataka kuwa na moyo wa uvumilivu na subira wakati huu wanapoomboleza vifo vya wapendwa wao. 
Aidha, Rais Kikwete amewaombea kwa Mungu waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo wapone haraka, ili waweze kuungana tena na ndugu na jamaa zao.

No comments: