MAJANGA TENA UDSM, MOTO WATEKETEZA BWENI LA WANAWAKE


Moto mkubwa uliozuka na kuteketeza sehemu ya bweni la wanawake katika Hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) zilizopo Mabibo jijini Dar es Salaam, uliibua taharuki kwa wanachuo na wananchi waishio jirani na eneo hilo.

Katika tukio hilo, mbali ya moto kuunguza mali za wanafunzi, wawili kati ya wanafunzi wa kike walikimbizwa hospitali baada ya kuumia katika purukushani za kujiokoa ambapo mmoja alijirusha kutoka ghorofa ya pili ulipoanzia moto huo na mwingine aliumia kwenye mkanyagano wakati wa kujiokoa.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa chuo hicho kikongwe na chenye heshima ya miaka mingi barani Afrika, Profesa Rwekaza Mukandala alisema hakuna mwanafunzi aliyepoteza maisha kutokana na mkasa wa moto huo ulioanza majira ya saa 3 asubuhi katika ghorofa ya tatu katika jengo la Block B, isipokuwa wanafunzi wawili walioumia baada ya kuruka.
“Tunashukuru Mungu hakuna aliyepoteza maisha ingawa kuna wanafunzi wawili wamejeruhiwa na tumewakimbiza hospitali. Ila mali nyingi za wanafunzi zimeharibika vibaya.
“Moto umetokea na tunahisi kuwa ni hitilafu ya umeme, lakini tunasubiri taarifa ya wataalamu kutupa chanzo cha moto.”
Aliongeza kuwa, ghorofa ya tatu ambayo ndiyo iliyowaka moto imeharibika vibaya na kuwa uongozi wake umewatoa wanafunzi wote katika jengo hilo kwa sababu za kiusalama.
“Shida kubwa tunayoshughulika nayo ni kuhakikisha tunawapatia malazi wanafunzi wote waliokuwa kwenye jengo liliokumbwa na moto. Hawatakaa mpaka hapo wataalamu watakapotuambia kama jengo hilo ni salama kwa kuishi watu.
Jengo hilo lenye ghorofa tatu lina vyumba 153 ambapo kila chumba wanaishi kati ya wanafunzi wanne hadi nane.
Alisema pia uongozi wa chuo chake utafanya ukarabati katika mabweni yaliyoko ghorofa ya kwanza na ya pili, ambayo pamoja na kuwa hayakukumbwa na moto, milango ya vyumba ilivyunjwa ili kuondoa vitu vilivyokuwapo.
“Tutawasaidia wanafunzi wote, hawa ni wanetu, hata wale wenye shida binafsi tutawasaidia, kwani kila kitu chao kimepotea ikiwa ni pamoja na vifaa, vitabu na fedha,” alisema na kuongeza kuwa, ninaamini hitilafu ya umeme uliokatika usiku wa kuamkia siku ya jana na kurudi ghafla baadaye.
Hata hivyo, pamoja na athari ya moto, baadhi ya wanafunzi wamejikuta wakipoteza vifaa vyao kama kompyuta mpakato, fedha na hata simu baada ya kuibiwa na watu walioingia katika vyumba kwa kile kilichoonekana kama kwenda kutoa msaada katika janga la moto.
Katika eneo la tukio, wanafunzi hao wakionekana kupatwa na mshtuko, walielekeza lawama zao kwa Kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuchelewa kufika eneo la tukio licha ya kudaiwa kuarifiwa mapema.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi, wa kike na kiume katika hosteli hizo zenye uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 4,000 kwa wakati mmoja, walishirikiana kuuzima moto na kuokoa mali.
Hata gari la Zimamoto lilipowasili, tayari shughuli ya kuokoa mali na kuudhibiti moto ilikuwa imefanikiwa, ndipo askari wa kikosi hicho wakajikuta katika wakati mgumu kutokana na wanafunzi wenye hasira kuanza kuwazomea na kuwarushia mawe wakiwataka waondoke kabisa eneo hilo.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Gibson George alisema chanzo hakijajulikana, lakini moto huo ulisambaa maeneo mbalimbali ya jengo hilo haraka.
"Watu wa zimamoto tumewapigia simu  mapema sana ila wamechelewa kufika hadi muda huu (saa 4:30) ndio wamefika, tumejaribu kuuzima moto na umepungua kidogo japo bado unaendelea kwa baadhi ya vyumba," alisema.
Hakuna kiongozi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kinondoni aliyepatikana kuzungumzia tukio hilo, kwani hata Kamanda wake, Camillius Wambura alipotafutwa mara kadhaa kwa njia ya simu, hakupatikana.

No comments: