MADEREVA KUPELEKWA MAFUNZO YA MIEZI 6 KUZUIA AJALI

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia, amesema katika kudhibiti ajali za mara kwa mara nchini, Serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka na kuwapeleka madereva wote wa abiria katika masomo ya miezi sita ili wawe na uchungu wa maisha ya watu.

Pia ameitaka Serikali kuipitia Sheria vizuri na kuhakikisha kuwa madereva wote wazembe wanaosababisha ajali, wananyang’anywa leseni badala ya kuwapatia adhabu ndogo au kuwatoza faini.
Mbatia aliyasema hayo Dar es Salaam wakati alipozungumza na waandishi wa habari, kuhusu ajali iliyotokea juzi mkoani Iringa na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40 na wengine 20 kujeruhiwa vibaya.
“Napenda ieleweke ajali si mipango ya Mungu kama watu wanavyodai, ajali zinapotokea huwa na sababu ikiwemo uzembe, katika ile ajali ya jana (juzi), nitahakikisha wahusika wote wanawajibika,” alisema.
Alisema suala la kuwapatia mafunzo madereva wanaoendesha hasa abiria ni la muhimu kutokana na ukweli kuwa madereva wengi wa sasa hawatambui thamani ya abiria waliowabeba.
Pamoja na hayo Mbatia aliwataka wabunge wenzake kuungana naye na kuihamasisha Serikali katika kuhakikisha mitandao ya reli inajengwa na kuboreshwa ili kuondokana na magari ya mizigo kutumia barabara moja na magari ya abiria.

No comments: