Aliyekuwa Waziri Mkuu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema
Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakijawahi kupata Katibu Mkuu hodari na mchapakazi
wa mfano wa Abdulrahman Kinana, tangu kuanzishwa kwake.
Katika hatua nyingine, Kinana akiwahutubia
wakazi wa mji wa Mto wa Mbu wilayani Monduli, alisisitiza kuwa uadilifu
utaendelea kuwa sifa namba moja ya mgombea wa CCM kwa nafasi yoyote ya uongozi,
na kwamba Watanzania wanaweza kusamehe kasoro nyingine, lakini si kwa kiongozi
kuwa mlaji na mdokozi wa mali ya umma.
Aidha, Katibu Mkuu huyo wa CCM amemwomba
Lowassa kusaidia kushawishi wabunge wenzake kushinikiza bungeni kubadilishwa
kwa sheria zote, zinazosababisha kero kwa wananchi, zikiwemo sheria
zilizorejesha kwa
mlango wa nyuma ushuru na kodi kero kwa wananchi,
ambazo awali zilifutwa na Serikali.
"WanaCCM wote nyie ni mashahidi, kazi
inayofanywa na Kinana na Nape (Nnauye- Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Itikadi na
Uenezi) ni kubwa na kwa kiasi kikubwa sana wamerejesha uhai wa chama chetu.
"Chini ya uongozi wa Kinana sasa CCM
imekuwa moja na kwa kiasi kikubwa amerejesha imani ya wanaCCM na wananchi wa
Tanzania kwa chama chao.
“Kazi anayoifanya ni kubwa na ngumu sana.
Kufanya mikutano 26 mfululizo si jambo rahisi hata kidogo na nimemweleza mke wangu
azungumze na mkewe, ili apunguze hizi safari," alisema Lowassa aliyekuwa
akishangiliwa na umati wa wananchi.
Akizungumza na wakazi wa Jimbo la Monduli,
Kinana pamoja na kusifu kile alichokiita kiwango cha juu cha utekelezaji wa
Ilani ya CCM kilichofanywa na Lowassa katika jimbo hilo, alisisitiza umuhimu wa
viongozi na wanachama wa CCM kuzingatia uadilifu katika utumishi wao kwa umma.
"Katika siku za hapo katikati, wananchi
walianza kupoteza imani kwa chama chetu kwa vile sisi wenyewe hatukuwa sawa,
tulikuwa hatutekelezi kile wananchi wanachohitaji, lakini sasa tumejipanga
vizuri katika kukisimamia chama chetu ipasavyo.
"Watanzania wa sasa hawapo tayari kuona
nchi yao inaongozwa kwa ujanja ujanja, au kwa watu kuwa walaji au wala rushwa.
Wapo tayari kukusamehe kosa jingine lolote, lakini si kwa suala la uadilifu,
wizi na udokozi wa mali ya umma au rushwa," alisema Kinana.
Kinana alitumia nafasi hiyo kumwomba Lowassa
kuisaidia CCM katika kushawishi wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kufuta au kufanyia marekebisho sheria zote zisizo na manufaa kwa
wananchi na hasa zile zinazosababisha kuibuka kwa kodi na ushuru kero
kwa wananchi.
"Sheria zinaundwa kwa manufaa ya wananchi
na si wanyama. Kama zipo sheria zinaifanya jamii ilalamike au inawapokonya
wananchi haki zao, basi sheria hiyo itakuwa haifai na ni vema ndugu yangu
Lowassa ukanisaidie katika kulishawishi Bunge kuzifuta sheria za aina
hii," alisema Kinana.
Akizungumza na wakazi hao wa Mto wa Mbu, Nape
alisema kazi iliyofanywa na Lowassa katika kuliletea maendeleo jimbo hilo ni
kubwa.
Pia, alitumia muda mrefu kusifu uadilifu,
uhodari na uchapakazi wa Mbunge wa zamani wa Jimbo hilo la Monduli na Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Sokoine, kuwa akishirikiana na viongozi wengine,
alijenga misingi ya kuwafanya viongozi wa umma kuwa waadilifu na jasiri katika
kufikia uamuzi kwa masuala ya kitaifa.
No comments:
Post a Comment