Hatima ya
tuhuma za Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na wenzake kuhusu fedha
walizopata kutoka iliyokuwa akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu
(BoT), itapelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete.
Ofisa Sheria Mkuu
wa Sekretarieti ya Maadili, Filotheus Manula, ameliambia mwandishi kuwa, baada
ya Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kukusanya tuhuma
pamoja na utetezi wa pande zote mbili, limeandika ripoti na utetezi na
kuuwasilisha kwa Rais ambaye ndiye mwenye maamuzi ya kutoa hukumu.
Alisema wao wamemaliza vikao vyao na
kinachoendelea ni kuandaa ripoti ambayo baraza hilo litaeleza kwa nini liliamua
kumpeleka mshitakiwa ndani ya baraza na mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa
pamoja na utetezi wa watuhumiwa hao.
“Baada ya
kupeleka majumuisho yetu, uamuzi wa hukumu uko kwa Rais kwani baraza halina
uwezo wa kutoa hukumu na ndiyo inavyofanyika kwa miaka yote,” alisema.
Chenge alipanda
katika kizimba cha Baraza la Maadili, kujibu mashitaka ya kutumia madaraka yake
vibaya alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kushauri Serikali iingie
mkataba wa miaka 20 na kampuni ya IPTL.
Aidha, anadaiwa
baada ya kustaafu wadhifa huo wa uanasheria wa Serikali Desemba 24, mwaka 2005,
mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa mshauri mwelekezi wa kampuni wa VIP
Engineering and Marketing Limited iliyokuwa na hisa za asilimia 30 kwenye
kampuni ya IPTL na kujipatia Sh bilioni 1.6.
Baada ya
kusomewa mashitaka hayo, mbunge huyo alikataa kesi hiyo kusikilizwa na
kuwasilisha pingamizi la kutaka suala hilo kutoendelea kusikilizwa kwa kuwa
tayari kuna kesi ya msingi Mahakama Kuu inayoendelea kusikilizwa.
Naye Profesa Anna Tibaijuka, aliitwa katika Baraza
la Maadili kwa viongozi wa umma kujibu
tuhuma za kukiuka maadili ya uongozi na kujipatia Sh bilioni 1.6 ambazo
aligawiwa kutoka katika fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo,
Profesa Tibaijuka alikana mashitaka hayo, na kusisitiza kuwa hakukiuka maadili
hayo ya viongozi wa umma, kwa kuwa fedha hizo hakuziomba kwa maslahi yake
binafsi, bali kwa ajili ya kuendeleza na kuboresha taasisi yake inayotoa huduma
ya elimu kwa watoto wa kike wasio na uwezo lakini wenye vipaji.
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, alikiri
mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kwamba, aliomba na Sh milioni 40.4, kutoka kwa James Rugemalira
kwa kujitetea, alifanya hivyo kama ilivyo kawaida pia kwa wabunge wengine.
Ngeleja alidai
mbele ya baraza hilo kwamba, msaada huo aliopewa na Rugemalira, hauna tofauti
na mingine aliyowahi kupokea kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa kama vile
Reginald Mengi, Said Salim Bakhresa na Yusuf Manji.
Wengine ambao
taarifa zao zitapelekwa kwa Kikwete, ni Mnikulu Shaban Gurumo, Mkurugenzi wa
Sheria wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa
Mujunangoma, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Ufilisi na Udhamini (RITA),
Philip Saliboko, Naibu Kamishna
Upelelezi na Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Loicy Appollo.
Pia yumo Mkurugenzi Mdhibiti
Uchumi Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Dk Benedict Diu na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora,
Gulam Remtullah.
No comments:
Post a Comment