BENKI YA WALIMU KUANZA KUUZA HISA MACHI 23


Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kinakusudia kuanzisha benki yake kwa kishindo, hivyo kuwataka walimu na wananchi kujitokeza kununua hisa za benki ya walimu.

Uuzaji wa hisa hizo unatarajiwa kufanyika kuanzia Machi 23 hadi Mei 4 mwaka huu baada ya taratibu za ufunguzi wa benki hiyo kufikia hatua za mwisho.
Akizungumza Rais CWT, Gratian Mukoba (pichani) alisema maombi ya kuuzwa kwa hisa hizo yameshakubaliwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), hivyo waraka wa matarajio utatolewa na kusambazwa nchi nzima mwezi huu kabla ya mauzo kuanza.
Alisema  baada  ya kupata kibali hicho, benki hiyo itaanza na mtaji mkubwa unaozidi Sh bilioni 25, kwani mtaji wa chini wa kuanzisha benki ya biashara hapa nchini ni  Sh bilioni 15.
Aliongeza kuwa hisa hizo, zitauzwa kwa wiki sita na baada ya hapo majina ya wanahisa yatapelekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya uhakiki na benki kupatiwa leseni yake, ianze biashara na hisa zitaorodheshwa kwenye Soko la Hisa Juni mwaka huu.
Aidha,  chama hicho kimeweka kivutio kwa walimu cha Sh 50,000 kwa kila aliye hai katika malipo yake kwa chama. Hali hiyo itawawezesha kununua hisa 100 katika benki, ambacho ndicho kiwango cha chini, hivyo kuwataka walimu wanunue hisa kwa wingi ili kuongeza mtaji wa benki.
Alisema ili kuhakikisha uuzaji wa hisa unamfikia kila Mtanzania wameamua kuweka utaratibu wa kununua kwa njia ya simu za mkononi kwa kushirikiana na kampuni ya MaxMalipo na kwenye ofisi za madalali wa soko la hisa na matawi yote ya benki ya CRDB  nchi nzima.
Aidha, alisema mpaka sasa walimu waliopo ni zaidi ya 200,000 na lengo lao likiwa ni watu 300,000, ambao ni walimu na wananchi wa kawaida.
Pia, aliomba wanachama wa chama hicho na wananchi wajitayarishe ili ifikapo Machi 23, waanze kununua hisa kwa wingi ili kumiliki benki hiyo kwa faida ya nchi.

No comments: