Abiria 57 wa basi la Osaka lililokuwa linatoka
Bukoba kwenda Dar es Salaam wamenusurika
kifo baada ya basi hilo kugonga tela la lori lililokuwa limeegeshwa kutokana na
kuwa bovu na kutumbukia mtaroni.
Ajali hiyo iliyotokea katika barabara kuu
Dodoma/Morogoro eneo la Chuo cha Biashara (CBE) Kata ya Makole Manispaa ya
Dodoma kwenye makutano ya barabara maarufu kama kona ya Dodoma Inn, majira
yanayokaribia saa sita usiku.
Imeelezwa kuwa dereva wa basi hilo lenye namba za
usajili T. 197 BUS Scania, Said Chaupendo Mshana (33) aligonga tela hilo lenye
namba za usajili T. 533 BNM la gari lenye namba za usajili T. 426 BMJ Scania
lililokuwa likiendeshwa na Idd Juma (41) lililokuwa limeharibika, kabla
hajatumbukia mtaroni na kujeruhi abiria mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime
alisema kwamba basi hilo la Osaka baada ya kushusha abiria stendi kuu ya mabasi
Dodoma liliondoka likiwa katika mwendokasi na kushindwa kusimama pamoja na kusimamishwa
na askari wa usalama barabarani waliokuwa kwenye eneo ambalo lori limeharibika.
“Kutokana na mwendokasi, aliligonga tela kisha kutumbukia mtaroni pembeni mwa
barabara katika uzio wa Chuo cha Biashara (CBE) na kusababisha majeruhi kwa
abiria mmoja aliyefahamika kwa jina la Justa Trazias mwenye miaka 19, mkazi wa Ubungo River side Dare es Salaam
ambaye amelazwa katika hospitali
ya rufaa Dodoma kwa matibabu na hali yake
inaendelea vizuri,” alisema Kamanda Misime.
Kamanda Misime alisema uchunguzi wa awali unaonesha
kwamba chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva, mwendokasi na kukataa kutii
amri ya askari aliposimamishwa kisha kushindwa kulimudu gari na kusababisha
ajali hiyo.
Kamanda huyo ametoa mwito kwa madereva kuwa na
udereva wa kujihami na wenye kuchukua tahadhari na kufuata sheria kwa kutokiuka
agizo la mabasi kutotembea baada ya saa sita usiku.
“Kwa muda
huo alitakiwa walale stendi ya mabasi Dodoma na ndiyo maana aliposimamishwa na
askari alikataa kusimama na matokeo yake akasababisha ajali hii,” alisema
Kamanda Misime.
No comments:
Post a Comment