AMCHINJA MPWA WAKE, NAYE AUAWA KWA KUCHOMWA MOTO MBEYA


Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wakazi wa Mtaa za Nsalaga jijini Mbeya, asubuhi wameshuhudia matukio ya mauaji ya watu wawili ndugu, moja likiwa ni mtu aliyemchinja na kumtenganisha kichwa na kiwiliwili mtoto wa dada yake, kabla naye kuuawa kwa kupigwa mawe na kisha mwili wake kuchomwa moto.

Yonah Mwamwele (38), ndiye aliyekuwa wa kwanza kumuua mtoto Johnson Mwamwele (5) mtoto wa dada yake kwa kutumia sululu.
Lakini ghafla, naye alijikuta akivamiwa na kundi la watu wenye hasira na kuanza kumshambulia kwa ngumi na silaha za jadi yakiwemo mawe hadi kumtoa uhai, na kisha kuuteketeza kwa moto mwili wake.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi aliyesema tukio la kwanza lilitokea jana saa 5:30 asubuhi katika eneo hilo la Nsalaga.
Msangi alisema kabla ya kumuua mpwa wake, Mwamwele alikuwa anamkimbiza mtoto huyo aliyekuja kubainika kuwa ni wa dada yake ambaye aliamua kukimbilia kwenye nyumba inayoendelea kujengwa iliyopo mtaani hapo, ambapo ndani yake walikuwepo mafundi wakiendelea na ujenzi.
“Mafundi walipomuona mtoto huyo akiingia na kufuatiwa na Mwamwele, walijaribu kumsihi ili amuache mtoto huyo, lakini aliwatishia  sululu aliyokuwa ameishika mkononi ambapo mafundi hao waliogopa na kurudi nyuma ambapo alipata nafasi ya kuingia ndani," alisema Msangi.
Kwa mujibu wa Msangi, mara baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo, Mwamwele  alimfuata moja kwa moja mtoto huyo na kumpiga kwa sululu shingoni na kufanikiwa kutenganisha kichwa na kiwiliwili cha mtoto huyo aliyeaga dunia papo hapo.
Aliongeza mafundi baada ya kuona hali hiyo, walianza kupiga mayowe ya kuomba msaada, ambapo ghafla kundi kubwa la watu lilijitokeza na kuanza kumfukuza Mwamwele ambapo walifanikiwa kumkamata na kuanza kumpiga na baadaye waliamua kumchoma moto hadi kuteketea na polisi walipofika eneo la tukio walimkuta tayari ameaga dunia.
Kamanda Msangi alisema baada ya kukamilisha kufanya mauaji hayo ya Mwamwele, wananchi hao wenye hasira walirudi kwenye nyumba alimofia mtoto Johnson na kuanza kuipiga mawe huku wakivunja vioo vya nyumba hiyo kwa mawe, sababu kuwa ikielezwa wahusika walishindwa kutoa msaada kwa mtoto aliyeuawa.
Alisema upelelezi unaendelea ili kuweza kutambua kiini cha Mwamwele kuamua kumfukuza mtoto huyo wa dada yake na kisha kumuua kinyama kwa sululu.
*Picha ya Maktaba.

No comments: