YANGA YASONGA MBELE KOMBE LA SHIRIKISHO, AZAM KIBARUANI LEO


Yanga imeingia raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika licha ya kufungwa mabao 2-1 na BDF XI ya Botswana katika mechi ya marudiano ya raundi ya awali usiku wa kuamkia leo mjini Gaborone.

Kwa matokeo hayo, Yanga imesonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya ushindi wake wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Februari14, mwaka huu.
Sasa vijana hao wa Hans van Pluijm watakutana na mshindi kati ya Sofapaka ya Kenya na Platinum ya Zimbabwe ambazo zinarudiana wikiendi hii. Katika mechi ya kwanza nchini Kenya, wenyeji walifungwa mabao 2-1.
Katika mechi hiyo iliyooneshwa na kituo cha televisheni cha Azam Two, Yanga jana usiku walikuwa wa kwanza kupata bao katika kipindi cha kwanza wakati mshambuliaji wake nyota, Mrisho Ngassa alipofunga bao hilo katika dakika ya 29.
Kwenye Uwanja wa Lobatse, Ngassa alifunga bao hilo kwa kuunganisha kwa kichwa pasi ya Amisi Tambwe, baada ya  krosi safi iliyochongwa na Simon Msuva kutemwa na kipa wa BDF XI, Agnecious Tebagano.
Yanga iliuanza mchezo kwa kasi na dakika ya tatu, Ngassa alipoteza nafasi ya wazi baada ya beki wa BDF XI, Polontle Lerole kuukosa mpira mrefu uliopigwa na Oscar Joshua na Ngassa kubaki na kipa, lakini shuti alilopiga lilikwenda nje.
Yanga iliendelea kuutawala mchezo kwa kucheza kwa kasi huku ikipanga vyema mashambulizi yao, lakini wenyeji walizinduka na kufanya shambulizi kali katika dakika ya 14, ambalo Bonolo Phuduhudu alipiga shuti kali lililopaa juu ya lango la Yanga.
Kasi ya wachezaji wa Yanga ilionekana kuwazidi wenyeji BDF XI, na kuwalazimu kuanza kucheza rafu na dakika ya 16 Mosha Gaolaolwe alioneshwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Juma Abdul na dakika nne baadaye wenyeji walilazimika kucheza baada ya Othusitse Mpharitlhe kuoneshwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mbaya Msuva.
Mshambuliaji wa Yanga, Dan Mrwanda naye alioneshwa kadi ya njano dakika ya 26, kwa kuchezea vibaya Mastar Masitara, nje kidogo ya lango lake, lakini BDF XI, walishindwa kutumia vyema nafasi hiyo.
Yanga waliongeza mashambulizi kwenye lango la wapinzani wao BDF na katika dakika ya 45, Msuva alikaribia kuifungia Yanga bao la pili baada ya kupiga kichwa kilichogonga mwamba wa juu na kutoka nje.
Kipindi cha pili wenyeji walikianza kwa kasi na kuwabana Yanga kwa kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la wageni wao na kupata bao la kusawazisha kupitia kwa Morcient Mosimonyane katika dakika ya 49.
Bao hilo lilionekana kuwachanganya wachezaji wa Yanga na kuanza kucheza kwa kujihami na kuwaacha BDF XI, kuutawala mchezo huku wakifanya mashambulizi mengi kwenye lango lao na kupoteza nafasi kadhaa walizozipata.
Katika dakika ya 73, Mrwanda alitolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kupewa kadi ya pili ya njano baada ya kumchezea rafu kiungo wa BDF XI, Master na kufanya timu zote mbili kucheza wakiwa pungufu.
Wenyeji walizidi kuongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la Yanga ambao muda mwingi walikuwa wakipoteza muda na katika dakika ya 86, Kumbulani Madziba, aliifungia bao la pili baada ya kichwa alichopiga kugonga mwamba wa juu na mpira kumkuta tena na kuumalizia wavuni huku mabeki wa Yanga wakishindwa kuuondosha kwenye hatari.
Yanga: Ally Mustapha, Abdul, Joshua, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Mbuyu Twite, Msuva, Haruna Niyonzima,  Ngassa/Kpah Sherman, Tambwe na Mrwanda.
Wakati Yanga ikimaliza shughuli yake jana usiku, mabingwa wa Tanzania Bara, wao leo wanashuka dimbani ugenini nchini Sudan kuvaana na wenyeji El Merreikh katika marudiano ya mechi ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa.
Azam FC wanacheza wakiwa tayari na faida ya mabao 2-0 waliyofunga katika mchezo wa awali uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi wiki mbili zilizopita.
Kutokana na ushindi wake huo, ikiwa watatoka sare katika mchezo wa leo, watazidi kusonga mbele kwa hatua nyingine, lakini kama watafungwa mabao zaidi ya hayo watatolewa kwenye mashindano hayo.
El Merreikh sio wageni wa michuano hiyo, huwa hawatabiriki wakati wowote wanaweza kubadilisha matokeo kama Azam FC hawatakuwa makini.
Tangu Azam FC waingie Sudan mapema wiki hii, wamekutana na vitimbwi kuanzia kwenye hatua ya mapokezi ambako ilidaiwa walipokewa na basi kuukuu, hiyo yote ni kutaka kuwavuruga kisaikolojia ili wafanye vibaya leo.
El Merreikh hudaiwa wanaweza kufanya lolote ilimradi waifunge Azam FC katika mchezo huo, lakini Azam hawatakiwi kuogopa au kutishwa na vitimbi vya aina hiyo kwa vile hufanyika kwa nia tu ya kuwavuruga.
Azam FC wakati mwingine huwa hawaeleweki na kuna wakati hubadilika na kubadili matokeo.
Katika michezo yao miwili iliyopita ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hawakucheza kwa kiwango kizuri pengine walikuwa wakicheza kwa tahadhari kwa kuhofu wasipate majeruhi wengi.
Katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ugenini Mlandizi mkoani Pwani, walitoka sare ya bila kufungana wakati dhidi ya Tanzania Prisons, matokeo yalikuwa hivyo pia, kwenye uwanja wao wa Azam Complex.
Kocha wa Azam FC, Joseph Omog alionesha dhahiri kuwa nguvu zao walizielekeza katika mchezo wa leo, kwa kuonesha kiwango kama kile cha awali kuhakikisha wanaondoka na ushindi au sare.
Nyota wanaotegemewa katika mchezo huo ni Kipre Tchetche, Brian Majwega, Didier Kavumbagu, Pashal Wawa na Salum Abubakar waliocheza kwa ushirikiano mkubwa katika mchezo wa awali na kuiwezesha timu yao kushinda.

No comments: