YANGA YAISAMBARATISHA MTIBWA SUGAR 2-0 NA KUKAA KILELENI

Timu ya soka ya Yanga imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kuifumua Mtibwa Sugar mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.

Katika mchezo huo mkali na wakuvutia uliochezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo wa Dar es Salaam akisaidiwa na John Kanyenye wa Mbeya na Josephat Bulali wa Tanga, ulishuhudia miamba hiyo ikienda mapumziko bila kufungana licha ya kosakosa nyingi hasa kwa upande wa Yanga kupitia kwa Simon Msuva na Amisi Tambwe.
Katika dakika ya 39, Yanga ilipata pigo baada ya beki wa kushoto Edward Charles kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Abdul.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Yanga ikitawala kwa kiasi kikubwa na kuelekeza mashambulizi makali langoni mwa Mtibwa lakini umakini wa safu ya ulinzi ya timu hiyo ukaweza kudhibiti madhara yasiweze kutokea langoni mwao.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Yanga, Hans van Pluijm kumtoa Kpah Sherman na kumuingiza Mrisho Ngassa yalibadilisha kabisa sura ya mchezo huo na kuliweka lango la wapinzani wao katika hali ngumu ndani ya dakika saba za mwanzo.
Dakika ya 53, Ngassa almanusura aipatie timu yake bao baada ya mpira aliopiga kugonga mwamba wa juu wa lango la Mtibwa.
Dakika mbili baadaye, Ngassa alisawazisha makosa na kufanikiwa kuiandikia Yanga bao la kwanza baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Msuva kuwatoka mabeki wa Mtibwa na kumimina krosi safi iliyomkuta mfungaji.
Wakati Mtibwa wakiendelea kujiuliza, Ngassa tena akaiandikia Yanga bao la pili katika dakika ya 62 akitumia vema pasi aliyotanguliziwa na Haruna Niyonzima na kisha kuwazidi mbio mabeki wa Mtibwa kabla ya kumpiga chenga kipa Said Mohammed na kufunga kwa urahisi.
Baada ya bao hilo, Yanga ikatawala kwa kiasi kikubwa mchezo huo wakitumia nafasi ya wachezaji wa Mtibwa ambao walionekana dhahiri kuchanganyikiwa na kukata tamaa hali iliyowafanya kukoswakoswa mabao mengine.
Kwa matokeo hayo, Yanga sasa imefikisha pointi 25 baada ya kushuka dimbani mara 13 na kuiacha Azam ikishika nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi zake 22 kutokana na mechi 12 ilizocheza.
Yanga iliwakilishwa na Ally Mustapha, Mbuyu Twite, Edward Charles/Juma Abdul (dk 39), Rajab Zahir, Nadir Haroub, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amisi Tambwe, Kpah Sherman/Mrisho Ngassa (dk 53) na Andrey Coutinho.
Mtibwa: Said Mohamed, Andrew Vincent, David Luhende, Ally Lundenga, Salim Mbonde, Shaaban Nditi, Ally Shariff/Ramadhani Kichuya (dk 62), Henry Joseph, Ame Ally, Ibrahim Rajab Jeba/Mohammed Ibrahim (dk 27) na Jamal Mnyate/Vincent Barnabas (dk 60).

No comments: