Wasafiri kutoka Tanzania kwenda India kwa shughuli za matibabu na biashara
wataruhusiwa kupata visa wafikapo nchini
humo.
Hayo yalisemwa na Balozi wa India nchini,
Debnath Shaw wakati akijibu maswali ya wafanyabiashara wa kitanzania wakati wa
mkutano baina ya wafanyabiashara wa ndani na wenzao kutoka jimbo la Gujarat
India.
Alisema: “Tutahakikisha tunafanya utaratibu
huo na utaanza siku za usoni ili kupunguza usumbufu wanaoupata Watanzania
waendao India”.
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu Mtendaji wa
Global Investors Consultstion Center
(GICC), Shainul Bhanji alisema kutokana na ripoti ya Benki ya Dunia Tanzania
imeonekana kuwa ni nchi yenye mazingira mazuri ya biashara kwani ripoti
inaonesha Tanzania inaendelea kushika nafasi nzuri ukilinganishwa na nchi
jirani za Kenya na Uganda.
“Tanzania ilikuwa nafasi ya 142 kati ya 180 kwa mwaka 2011 lakini sasa
imepanda hadi nafasi ya 131 huku Kenya
ikiwa katika nafasi ya 136 na Uganda nafasi ya 132,” alisema Bhanji.
Naye Rais wa Taasisi ya Wenye Viwanda toka
Jimbo la Gujarat India Amit Patel alisema kwa sasa India ni nchi ya nne kwa
ukubwa kwa nchi zinazofanyabiashara kwa Afrika na wana uhakika kuwa
watafanyabiashara kuzidi China, Marekani na Ulaya.
Alisema Serikali ya India imeahidi kutoa
mikopo ya masharti nafuu ya bilioni 6 mwaka huu kwa nchi za Afrika ili
kuboresha miundombinu na mazingira ya kufanyabiashara.
Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara, wakulima
na wenye viwanda nchini Francis Lukwaro alisema mkutano utasaidia
wafanyabiashara wa Tanzania kujifunza mambo mapya ya kibiashara kutoka India.
Alisema kwa upande wa Tanzania kuna mengi ya
kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara hawa kwani wengi wao ni wafanyabiashara
wakubwa na wameendelea.
No comments:
Post a Comment