WATAKA SUMATRA IBANWE IPUNGUZE NAULIChama cha Kutetea Abiria Tanzania (CHAKUA)  kimewaomba Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sita kuingilia kati na kuagiza  Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), isikilize kilio cha wananchi  kuhusu kupunguzwa kwa nauli.

Hayo yalisemwa jana na mwenyekiti  wa chama hicho, Hassan Mchanjama wakati akizungumza na waandishi wa habari jiji Dar es Salaam.
Alisema wamefikia uamuzi huo baada ya Ewura kushusha bei ya mafuta, hivyo ni vyema na abiria nao wakanufaika kutokana na mafuta kushuka tangu mwaka jana Desemba, kwani inaonekana wanaonufaika ni wamiliki wa vyombo vya usafiri.
Aliongeza kuwa imekua ikishuhudiwa mara kwa mara mafuta yakipanda kidogo, nauli nazo zinapanda haraka, lakini mafuta yakishuka  Sumatra hawataki kuitisha mkutano na wadau ili kujadili kushusha nauli .
“Sisi Chakua tumechukua hatua ya kwanza kuwaandikia barua, lakini Sumatra ipo kimya tukaandika tena Februari 5, lakini bado wamekaa kimya,” alisema Mchanjama.
Alisema Chakua inataka nauli zote zipungue kwa asilimia 25, kwa mfano nauli za daladala chini ya kilometa 10 nauli ya sasa ni Sh 400 hivyo ipungue hadi Sh 300 na mikoani nauli ipungue kwa asilimia 25.
Alisema nauli ikipungua itasaidia kupunguza bei za bidhaa nyingine ikiwemo vyakula, kwani mfumko wa bei unachangiwa na gharama za usafirishaji.
Katibu wa Barabara wa chama hicho, Gervas Rutaguzinda aliitaka serikali kujenga vibanda vya kupumzikia abiria katika Kituo  Kikuu cha Mabasi  Ubungo, kwani kila abiria anayeingia katika kituo hicho analipa Sh 200. Alisema pesa zinazokusanywa kila siku na kituo hicho ni nyingi, lakini kwamba hakuna vibanda muda mrefu.
“Abiria wananyimwa haki wanakaa kwenye jua kali na mvua hakuna pa kusimama wakati wanalipa kiingilio ni jambo la aibu na lazima watakuwa wanajiuliza ni wapi fedha hizo zinapelekwa wakati hakuna maendeleo yoyote,” alisema Rutaguzinda.

No comments: