WAMACHINGA WATAJIRISHA WATU, JANGWANI KUGEUZWA GULIO



Wakati serikali ikianza kutafuta suluhisho  la kudumu la matatizo wafanyabiashara ndogo, mama lishe kuhusu upatikanaji wa maeneo, imebainika kuwapo mchezo ‘mchafu’ wa wafanyabiashara wakubwa kutumia mgongo wa wamachinga,  kusambaza na kuuza  bidhaa zao maeneo yasiyoruhusiwa. 

Katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam,  imebainika yako maghala 12 ya bidhaa za chakula eneo la Ubungo, ambako wafanyabiashara ndogo wamekuwa wakigawiwa bidhaa kuziuza maeneo yasiyoruhusiwa na kisha jioni hupeleka hesabu kwa matajiri kwa ujira mdogo.
Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera alisema wamebaini tatizo hilo na wanapaswa kulizingatia wakati wa kutekeleza mpango wa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wa kusaidia wamachinga kufanya biashara zao kwa amani kwenye maeneo yanayoruhusiwa.
Aidha, katika kutekeleza azma hiyo ya Tamisemi, Manipsaa ya Ilala  imeainisha maeneo kadhaa, ikiwemo Viwanja vya  Jangwani ambako itajengwa miundombinu kama vile vyoo, taa na kuwekewa ulinzi,  litumike kwa ajili ya soko la kila siku.
Hatua hizo za halmashauri za jijini Dar es Salaam,  ni utekelezaji kwa vitendo mpango aliosema Waziri Mkuu,  Mizengo Pinda katika mkutano wa 18 wa Bunge ulioahirishwa hivi karibuni.
Pinda alisema kimeundwa  kikosi cha kiofisi kitakachohusisha wajasiriamali hao kwa lengo la kukubaliana kuhusu maeneo na muda muafaka wa kuendesha shughuli zao. Wameanzia jiji la Dar es Salaam kabla ya kwenda miji na majiji mengine.
Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Mhowera alisema, “tumebaini wengi wa wanaofanya biashara maeneo yasiyoruhusiwa siyo wamachinga, bali ni vibaraka wa wafanyabiashara wakubwa wenye maduka na maghala makubwa.”
“Mfano pale Ubungo, tumebaini kuna maghala 12, ya wafanyabiashara wanaotoa bidhaa za mazao ya chakula mikoani na wanawaajiri watu ambao kila siku huenda kwenye maghala hayo kuchukua bidhaa na kuzipanga barabarani na jioni hurudisha hesabu kwa ujira mdogo, sasa hao ni machinga kweli?” alisema Mhowera.
Alisema iko haja ya kuchukua hatua kudhibiti wafanyabiashara wakubwa  wanaofanya mbinu chafu ionekane ni machinga  na hivyo kukwepa kuuza kwenye masoko kisheria.
Alisema wanafahamu yaliko maghala hayo. Alisema katika utekelezaji wa azma ya kusaidia wafanyabiashara ndogo, watahakikisha watu hao wanatenganishwa, kwani wanatumia mgongo wa wamachinga kuongeza tatizo la watu kufanya biashara kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kwa manufaa yao.
Ofisa huyo wa manispaa alisema walifanya utafiti kwenye maeneo yote, ambayo watu hufanya biashara barabarani na kubaini wapo wafanyabiashara wasio rasmi zaidi ya  3,400 .
Utafiti ulibaini wengi wao walipewa maeneo kwenye vizimba katika masoko mbalimbali yanayokubalika  kisheria kufanyia biashara ingawa baadhi yao, wanaendelea kufanya biashara maeneo.
 “Mifano ni mingi.., kuna mama mmoja (alimtaja jina)  huyu tulimbaini na tulikuwa naye wakati tunafanya tathimini ya wanaofanya biashara maeneo holela na yeye tulimgawia eneo Soko la Makumbusho na pia  ana eneo Soko la Shekilango, ila bado yuko barabarani pale Ubungo, ndio anajiita Mwenyekiti wa wafanyabiashara maeneo yasiyoruhusiwa.
“Na sasa anataka apewe tena eneo tulilotenga la soko pale Kituo cha Mabasi cha Mawasiliano, sasa utasema na huyo naye ni eneo kakosa”, alisema Mhowera.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngulumi alisema kwa upande wao wameanza utekelezaji kwa kutenga maeneo kwa kuzingatia upatikanaji wa wateja, ulinzi, miundombinu na usalama.
Alisema viwanja vya  Jangwani kwa upande wa mmoja wa karibu na Klabu ya Yanga, vitatumika kwa soko la kila siku na litajengewa miundombinu muhimu kama vile taa, vyoo na kuwekewa ulinzi.
Alisema pia siku zijazo, eneo hilo litajengwa maegesho ya magari ambayo wamiliki watapata fursa ya kununua bidhaa kabla ya kuondoka na magari yao.
“Kwa siku za usoni eneo la Jangwani litajengwa maegesho ya magari binafsi kwani hayataruhusiwa kuingia katikati ya mjini, na hiyo ni fursa kwa wafanyabiashara katika soko hilo kupata wateja,” alisema Mngulumi.
Alitaja maeneo mengine yaliyotengwa ni Chanika, Pugu, Kigogo Fresh, Mchikichini, Machinga Complex na Jangwani.
Alisema wanaendelea kufanya utafiti  wa maeneo mengine kuhakikisha wafanyabiashara wanaondoka kwenye maeneo hatarishi na kufanya biashara kwenye maeneo yanayoruhusiwa.
Alisema pia Manispaa inaimarisha Vyama vya Akiba na Mikopo (Saccos), viwe na mitaji mikubwa ya kukopesha wamachinga, waondokane  na kunufaisha wenye maduka ya bidhaa za jumla ambazo huuza kwa ujira mdogo.
 “Hatutaki tena machinga wafanye biashara kwa mali kauli ambayo mwisho wa siku anayefaidika ni mwenye mali na siyo machinga, tunataka wawezeshwe wawe na mitaji na wanunue wenyewe bidhaa zao na kuziuza kwa faida,” alisema Mngulumi.
Kwa upande wa Manispaa ya Temeke, msemaji wake, Joyce Msumba alisema wametenga masoko kila kata na pia eneo la Zakhiem limetengwa kwa ajili ya wafanyabiashara.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Jumanne Sagini alisema kila halmashauri ilipewa mwongozo wa kutenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo na vijana.
 “Tulitoa miongozi kwa halmashauri zetu zote nchini kutenga maeneo ya vijana na wafanyabiashara ndogo na wengi wametekeleza, ila wale waliotengwa kwenye maeneo hatarishi tumeyakataa kwani siyo salama, na utekelezaji wake tumewaambia uanze mara moja,” alisema Sagini.
Alisema Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Christopher Chiza,  ameshaanza kuchukua hatua kwa kuzungumza na wafanyabiashara ndogo kuangalia namna ya kuwasaidia.
Alisema serikali kwa kuona umuhimu, mfano kwenye kituo kipya cha mabasi madogo jijini Dar es Salaam cha Simu 2000 maarufu kama Mawasiliano, kumejengwa pia soko kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo.
Akizungumzia masoko ya Jumapili, Sagini alisema  yanafanyiwa utafiti yatakapotengwa yawe na miundombinu. Hata hivyo alisema masoko hayo hayatakuwa kila sehemu isipokuwa ni baada ya kupata tathmini nzuri ya maeneo.

No comments: