Serikali
imeagiza wakuu wote wa mikoa, kuweka mikakati ya kuhakikisha watoto wote
waliofaulu mitihani ya darasa la saba, wanajiunga na shule za sekondari katika
kipindi hiki kabla ya Machi 28 mwaka huu, vinginevyo watakaokwamisha watoto
hao watachukuliwa hatua kali.
Agizo
hilo limetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri MkuuTawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Kasimu Majaliwa katika kikao cha
Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Tabora (RCC), kilichoketi katika ukumbi wa Mtemi
Isike Mwanakiyungi mjini hapa juzi.
Alisema
kila mkoa unatakiwa kujiwekea mkakati wa kuhakikisha watoto wote,
waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule mbalimbali za sekondari wanaripoti
ili wasipoteze fursa hii muhimu waliyopata kwa kisingizio cha namna yoyote ile
iwe wazazi au vinginevyo.
‘Ili
zoezi hili liende vizuri na watoto wote waripoti kwa asilimia 100, suala la
usimamizi ni la muhimu sana na kila
halmashauri inapaswa kutekeleza wajibu wake ipasavyo, vinginevyo mtakuwa
mnakwamisha malengo ya serikali ya kufanikisha mpango wa matokeo makubwa sasa’,
aliongeza.
Aliagiza
wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na
wakurugenzi wa halmashauri zote, kuhakikisha kila mzazi au mlezi atakayehusika
kwa namna moja au nyingine kukwamisha au kuzuia mtoto wake kujiunga shule ya
sekondari, anachukuliwa hatua kali mara moja ikiwemo kufikishwa katika vyombo
vya sheria.
No comments:
Post a Comment