WAAFRIKA WAADHIMISHA MWAKA MPYA WA KICHINA

Waafrika wanaoishi na kusoma jijini hapa, wameshiriki na wenyeji katika sherehe za mwaka mpya wa China (Spring Festival) unaoadhimishwa kwa wiki moja kuanzia Februari 19 mwaka huu.

Walisherehekea mwishoni mwa wiki badala ya wakati husika kutokana na juma hilo kuwa na shughuli nyingi za China na pia watu wengi wakiwemo wenyeji husafiri nje ya miji kama Beijing kwa likizo muhimu ambayo wengi huipata mara moja kwa mwaka.
Sherehe hizo za Waafrika zilifanyika katika Kituo cha Kiafrika cha Beijing (BeijingAfrican Center) mjini hapa na kuhudhuriwa na watu mbalimbali kutoka mataifa ya Afrika na wenyeji Wachina.
Mratibu wa sherehe hizo na mwasisi wa kituo hicho, Tracy Qi ambaye ameishi Afrika Kusini kwa miaka 15, alisema lengo la sherehe hizo ni kuunganisha China na nchi za Afrika katika masuala muhimu ya kiutamaduni, kiuchumi na kijamii.
“Tunatengwa na mipaka ya kijiografia lakini sisi sote ni ndugu, nimeishi Afrika Kusini nusu ya maisha yangu nilionayo kwa sasa, nimefika Tanzania pia, hivyo ninawafahamu Waafrika walivyo wakarimu na wenye upendo, nia ya sherehe hizi ni kuwaleta watu pamoja, kufurahia na kujifunza tofauti zetu ili tuishi salama na kwa upendo,” alisema Qi.
Katika sherehe hizo, vyakula mbalimbali vya Kiafrika ikiwamo ugali, maharage, samaki, kisamvu, nyama za utumbo, sambusa, chapati na pilau pamoja na kahawa vilipikwa na wanafunzi wa Kiafrika kutoka Tanzania, Kenya, Msumbiji na Zimbabwe na kusababisha watu kugombea wakitaka kuhakikisha wanakula kila aina ya chakula cha Kiafrika. Kahawa iliandaliwa na wananchi wa Ethiopia.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mawasiliano cha China (CUC) na Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha Afrika chuoni hapo, Profesa  Zhang Yangiu aliyewaongoza wanafunzi wa Kiafrika kupika na kushiriki sherehe hizo, alisema ni fursa nzuri kujifunza utamaduni wa Kiafrika kwa kuwa nchi nyingi za Afrika ni rafiki wa kindugu wa China.
Nao wanafunzi wa CUC walioshiriki sherehe hizo, walisema kwa nyakati tofauti kuwa, wamejifunza mambo mengi na wakapendekeza kila mara kuwepo na hafla ya kuwakutanisha na wenyeji (Wachina) ili kueleza zaidi mazuri ya Afrika na kutoa nafasi ya wananchi wa China kulielewa Bara la Afrika zaidi.
“Fursa hii ni ya pekee, inapaswa kuendelezwa, tukutanishwe kwa mijadala, tuelezane masuala yanayotuhusu, tuifahamu China na Wachina wazifahamu nchi zetu maana wengi wanadhani Afrika ni nchi moja kumbe hawajui ni zaidi ya nchi 52,” alisema James Mwita kutoka Kenya.
Mwaka mpya wa China hufanyika kila mwaka kulingana na kalenda ya Kichina inayozingatia mwandamo wa mwezi. Katika sherehe hizo, masuala mbalimbali ya kiutamaduni hufanyika, hupikwa vyakula maalum huku kukiwa na mavazi ya rangi maalumu ya mwaka na watu hupeana zawadi, ikiwemo fedha kwa mtindo mbalimbali ukiwamo ule wa kuziweka katika miavuli.

No comments: