TANI 200,000 ZA SILAHA HARAMU ZATEKETEZWA

Tani 200,000 za silaha haramu zilizokuwa zimezagaa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) zimeteketezwa.

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa EAC, Richard Sezibera (pichani) mbele ya Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck  wakati alipozuru makao makuu ya jumuiya hiyo, jana.
Alisema silaha hizo zilizokamatwa kwa nyakati tofauti katika nchi mbalimbali za EAC  ni pamoja na mabomu tani  200.
Akizungumzia ujio wa Rais wa Ujermani katika makao makuu ya Jumuiya hiyo, Sezibera alikiri kufurahishwa na ujio huo na kusema kuwa utaongeza chachu ya nchi hiyo kuisaidia jumuiya hiyo.
Sezibera alisema mahitaji makubwa yanahitajika katika kufanikisha mahitaji ya wananchi wa EAC ikiwa ni pamoja na Afya, Mazingira, Miundombinu na vikundi vya akina mama na vijana wanachama wa jumuiya hiyo.
Naye Rais Gauck alizitaka nchi hizo kudumisha jumuiya hiyo na kuiboresha zaidi ikiwa ni njia mojawapo ya kuweka mshikamano kwa maslahi ya wananchi wake.
Alisema kuwa nchi ya Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya zitakuwa mstari wa mbele kuhakikisha zinatoa misaada kwa jumuiya hiyo bila ya kikwazo chochote.
Awali, Rais huyo alifanya ziara katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu iliyopo jijini Arusha kujionea utendaji kazi wa kila siku wa jumuiya hiyo na kujua changamoto zake.

No comments: