SUMATRA YAWAPIGA DARASA WAMILIKI WA MABASI YA MASAFA MAREFU

Mamlaka ya Udhibiti Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imewanoa wamiliki wa mabasi ya masafa marefu  kuhusu usimamizi na udhibiti wa sekta ya usafiri wa barabara ili wazaidie  kupunguza na kutokomeza kabisa ajali baada ya kuwapatia semina maalumu.

Semina hiyo maalumu ya siku mbili iliyoanza juzi mjini Morogoro imewashirikisha viongozi wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania ( TABOA) wakiongozwa na Mwenyekiti wao Taifa, Mohamed Hood, na kufunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka.
Dk Mwinjaka katika hotuba yake ya ufunguzi, aliwataka  wamiliki  wa mabasi kuwatumia madereva  wenye  weledi  ili kupunguza  ajali ikiwa na hatua ya kuwaendeleza kielimu katika vyuo  vya serikali  na vya ufundi stadi Veta.
Mbali na hayo, aliwataka wamiliki wa mabasi kushirikiana na vyombo vingine  kwa ajili ya kubaini mienendo ya madereva wao hasa suala la ulevi wanapokuwa kazini na mwendokasi, wakitambua  mabasi yao wameyanunua kwa gharama kubwa na pia yamebeba uhai wa maisha ya binadamu.
Hata hivyo, alisema aliwahakikishia wamiliki wa mabasi ya masafa marefu kuwa, Kamati iliyopewa jukumu ya kuangalia namna ya kurekebisha sheria za makosa yanayowahusu wamiliki na kwa madereva wao imefikia hatua nzuri na muda si mrefu utawekwa hadharani.
Pamoja na hayo, pia aliwataka wamiliki wa mabasi kuhakikisha  wanakuwa karibu kufuatilia kila jambo linalofanywa na dereva wake, kwani mwisho wa yote basi litabaki kuwa ni mali ya mmiliki na dereva ni mfanyakazi wake.
Naye Kamanda wa Kikosi  cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga  alisema  ajali za barabarani zinazohusisha  mabasi  hazitaweza  kupungua iwapo sheria  na kanuni  za mwaka 2007 kanuni 317 hazitazingatiwa  na wamiliki wa vyombo  hivyo  sambamba  na madreva  wao.
Naye  Mkurugenzi  Mkuu wa SUMATRA, Gilliard Ngewe, mada sita  ziliandaliwa na kutolewa kwa wamiliki wa mabasi ya masafa marefu, ikiwemo ya nafasi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri katika kuimarisha usalama barabarani sambamba na nyingine ya kanuni ya taratibu za uwasilishaji makalamiko.

No comments: