SUMATRA YATAFAKARI KUSHUSHA NAULI

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imewataka wananchi na jamii kuwa watulivu na kuendelea kuvuta subira, huku suala la kushuka kwa bei ya mafuta likifanyiwa utafiti ili kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua ya kushusha nauli za vyombo vya usafiri.

Akizungumza na mwandishi jana jijini Dar es Salaam, Meneja Leseni wa Sumatra, Leo Ngowi alisema tangu Mamlaka ya Udhitibi wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),kutangaza kushuka kwa bei ya bidhaa za mafuta nchini, wananchi wamekuwa wakihoji kwa nini bei za nauli nazo zisishuke.
Akizungumzia hilo, Ngowi alisema maoni ya wananchi na wadau wengine wameyasikia na kuwataka wawe watulivu kwani suala hilo linafanyiwa kazi ili kujiridhisha kabla ya kuchukua uamuzi wa kushusha nauli.
“Tunaomba wananchi wawe watulivu, wavute subira, suala hili tunalifanyia kazi, tunaangalia vitu vingi sio tu kushuka kwa bei ya matufa, bali pia na vitu vingine ili kujiridhisha na  tutapitia upya bei za nauli”, alisema Ngowi.
Aliongeza mamlaka hiyo imefurahi kushuka kwa bei ya mafuta na kwamba wataalamu wake wanaendelea kufanya uchunguzi sokoni ili kujiridhisha na bei za bidhaa kabla ya kufanya mabadiliko yoyote ya bei za nauli.
Awali juzi, watafiti mbalimbali wa masuala ya uchumi nchini walitoa maoni yao kwa kusema kushuka kwa mafuta kulipaswa kwenda sambamba na kushuka kwa bei ya bidhaa nyingine ikiwamo chakula na nauli.

No comments: