SIMBA YAWARARUA MAAFANDE WA PRISONS 5-0


Timu ya Simba leo jioni ilitoa kipigo kikali kwa Prisons ya Mbeya kwa kuibugiza mabao 5-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Ushindi huo mnono wa Simba umekuja wiki moja baada ya kupata kipigo cha bao 1-0 na Stand United mjini Shinyanga.
Katika mchezo huo, Simba walianza kuhesabu bao la kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake, Ibrahim Hajibu katika dakika ya 15 akiunganisha krosi nzuri ya Dan Sserunkuma.
Hajibu aliongeza bao la pili katika dakika ya 21 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na golikipa Mohammed Yussuf, aliyepangua shuti la Emmanuel Okwi kabla ya kufunga bao la tatu dakika ya 41 kwa mkwaju wa penalti.
Penalti hiyo ilitolewa baada ya beki wa Prisons, Lugano Mwangama kuunawa mpira kwenye eneo la hatari akiwa katika heka heka za kuokoa hatari langoni mwake.
Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi katika dakika ya 75 kwa shuti kali na Ramadhani Singano maarufu kama Messi akifunga dakika ya 84 na kuhitimisha karamu ya mabao kwa kikosi hicho.
Katika mchezo huo, Nurdin Chona wa Prisons alitolewa nje katika dakika ya 68 kwa kadi ya pili ya njano baada ya kumtolea maneno machafu mwamuzi.
Kwa ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi 23, baada ya kushuka dimbani mara 16, ikiwa nafasi ya nne nyuma ya Kagera Sugar yenye pointi 24, Azam FC pointi 27 na Yanga SC 31.
Simba: Ivo Mapunda, Hassan Kessy/Nassor Masoud Chollo', Mohammed Hussein Tshabalala, Hassan Isihaka, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano Messi, Said Ndemla, Dan Sserunkuma/Twaha Ibrahim Messi, Ibrahim Hajib/Awadh Juma na Emmanuel Okwi.
Prisons; Mohammed Yussuf, Lugano Mwangama, Laurian Mpalile, James Mwasote, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil/John Mathei, Adam Chimbongwe/Meshack Suleiman, Freddy Chudu, Ibrahim Isaka, Boniface Hau/Julius Kwanga na Godfrey Magetha.  

No comments: