SERIKALI KUAJIRI WALIMU WAPYA 35,000 MWAKA HUU


Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amesema Serikali imepanga kuajiri walimu zaidi ya 35,000 kwa ajili ya shule za sekondari, ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu nchini.

Alitoa kauli hiyo jioni wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Kiwere, baada ya kukagua ujenzi wa maabara na kuzindua nyumba nne za walimu kwenye Shule ya Sekondari ya Kiwere, tarafa ya Kalenga, wilayani Iringa.
Waziri Mkuu alisema walimu hao watagawanywa kwenye shule kulingana na mahitaji yaliyokwishawasilishwa na   watakapopata mgawo wao, hawana budi kuangalia kwanza shule zenye miundombinu iliyokamilika kama ilivyo kwa shule hiyo.
Akifafanua kuhusu kasi ya ujenzi wa maabara, Waziri Mkuu alisema: “Mkoa mzima wa Iringa unahitaji maabara 318 na zilizo tayari mpaka sasa ni 108.
“Lakini kuna nyingine 141 ambazo zimekwishaanza kujengwa na zimefikia hatua nzuri. Nimeambiwa katika muda mfupi ujao kutakuwa na maabara 249 zilizokamilika,” alisema.
“RC inabidi uwasukume watu wako ili hizi 69 ambazo hazijaanza kujengwa zikamilike kabla ya Juni mwaka huu kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete alivyoelekeza. Alisema hataongeza tena muda wa ujenzi,” aliongeza.
Alisema elimu ni sekta ya msingi ambayo Serikali imeamua kuipa umuhimu wa kipekee na kuiweka katika moja ya maeneo sita muhimu ya kipaumbele chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa ya Haraka (BRN).
Waziri Mkuu aliwataka wanafunzi wa shule hiyo wasome kwa bidii na wawe wasikivu, ili wafanye vizuri zaidi kwenye masomo yao.
Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Ofisa Elimu wa Wilaya ya Iringa, Leonard Msigwa, alisema ujenzi wa nyumba hizo nne zenye pande mbili, umegharimu Sh milioni 323.2. 
Alisema nyumba hizo zenye vyumba vitatu vya kulala, sebule na jiko, zina uwezo wa kubeba familia nane.
Msigwa alisema ujenzi wa nyumba hizo ulifanywa na shirika la Deswos la Ujerumani kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na wananchi.
Pia walisaidiwa kujengewa tangi la maji na mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 112 kila moja kwa ajili ya wasichana.
Akifafanua kuhusu hali ya ujenzi wa maabara, Ofisa Elimu huyo alisema hadi sasa wamekamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya Kemia na Bayoolojia, lakini bado viko kwenye hatua ya kupaka rangi. Aidha mfumo wa gesi na maji umekwishafungwa ndani ya vyumba vya maabara.
“Ujenzi wa maabara hadi sasa umekwisha gharimu Sh milioni 52.8/- na kwa Februari 2015, tumefanikiwa kutengeneza baadhi ya samani za maabara yaani meza 24 na stuli 96 zenye thamani ya Sh milioni 8.9,” alisema.

No comments: