PATO LA TAIFA SASA LAFIKIA TRILIONI 21


Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetangaza pato la taifa ambalo linaonesha kuwa thamani ya pato hilo katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka huu imefikia Sh trilioni 21.2.

Kiwango hicho kinaonesha ongezeko ikilinganishwa na Sh trilioni 19.8 za mwaka uliopita huku Sekta ya Madini ambayo imekuwa inafanya vizuri miaka iliyopita uzalishaji wake unazidi kuporomoka.
Katika takwimu hizo, kwa ujumla Pato la Taifa kwa bei ya mwaka 2007 linaonesha kuwa na jumla ya thamani ya Sh trilioni 10.7 mwaka jana ikilinganishwa na Sh trilioni 10.1 za mwaka juzi.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa NBS  Morris Oyuke (pichani) alisema takwimu hizo zinamaanisha  kuwa Pato la Taifa liliongezeka kwa kasi ya asilimia 6.8 katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2014 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 7.4 katika kipindi hicho mwaka 2013.
Kwa upande wa shughuli za uchumi za viwanda na ujenzi, Oyuke alisema uchimbaji madini ya dhahabu katika kipindi hicho ulishuka kutoka kilo 11,010 za mwaka juzi hadi kufikia kilo 10,137.
Shughuli za uchimbaji wa  mawe na kokoto ziliongezeka kwa kasi ya asilimia 5.2 katika kipindi hicho ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.3 ya mwaka juzi.
Tanzanite nayo inaendelea kuyumba kwani katika kipindi hicho kilo zilizozalishwa ni chache mno ikilinganishwa na kilo  zilizozalishwa mwaka juzi.
Kwenye sekta hiyo madini ya almasi imefanya vizuri kwani kiasi kilichozalishwa katika kipindi hicho mwaka jana kilikuwa ni karati 66,508 kutoka karati 27,828.
Kuhusu ukuaji wa Pato la Taifa kwa shughuli za kiuchumi, Oyuke alisema shughuli za kiuchumi za kilimo na mifugo zilikua kwa kasi ya asilimia 3.1 katika kipindi hicho ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 3.4. Takwimu hizo zinaonesha kuwa kilimo kiliporomoka.
Oyuke katika takwimu zake alisema katika kipindi hicho kilimo cha mazao kilikua kwa asilimia 2.4 ikilinganishwa na asilimia 4.5 mwaka juzi huku ukuaji wa shughuli za ufugaji ziliongezeka kwa asilimia 2.1 ikilinganishwa na asilimia 1.9. Kwenye kundi hilo ukuaji wa shughuli za misitu uliongezeka kwa asilimia 0.3 ikilinganishwa na asilimia 0.9 ya mwaka juzi.
Alisema ukuaji wa Sekta ya Kilimo na Mifugo ulitokana na jitihada za Serikali kuwasaidia wakulima kwa kutoa ruzuku na maelekezo ya maofisa ugani kwa wakulima kama vile kuchagua mbegu bora yalisaidia kuongeza uzalishaji.
Oyuke alisema uzalishaji wa viwandani ulikua kwa kasi ya asilimia 10.8 kutoka asilimia 10.4. Kasi ya ongezeko hilo kwa mujibu wa NBS ilitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa za vyakula, tumbaku, nguo na saruji.

No comments: