MUSWADA MAHAKAMA YA KADHI KUJADILIWA BUNGE LIJALO


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameeleza sababu za Bunge kushindwa kujadili miswada kadhaa, ikiwemo uliohusu Marekebisho ya Sheria ya Kiislamu, inayotambua Mahakama ya Kadhi.
 
Akihitimisha shughuli za mkutano wa 18 wa Bunge jana, Pinda alisema muswada huo umesogezwa mbele, ili Kamati ya Bunge ipate nafasi na muda wa kupitia na kutoa ushauri kwa Bunge.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 2 wa mwaka 2014, unaohusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria hiyo ya Kiislamu Sura 375 ni miongoni mwa ambayo haikujadiliwa.    
Mingine iliyopangwa kujadiliwa katika mkutano huo wa Bunge, ni  Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa mwaka 2014 na Muswada wa Sheria ya Takwimu wa mwaka 2013.   
“Hatukuweza kuijadili miswada hiyo katika mkutano huu, ili Kamati husika zipate nafasi na muda wa kupitia na kutoa ushauri kwa Bunge lako Tukufu.
“Ni matumaini yangu kwamba miswada hii itapata nafasi ya kuwasilishwa na kujadiliwa katika mkutano ujao wa 19 wa Bunge lako Tukufu,” alisema Pinda.   
Katika mkutano huo,  wabunge walipokea na kujadili taarifa mbalimbali zilizowasilishwa na Kamati za Bunge za kisekta na zisizo za kisekta.
Wakati huo huo katika hotuba yake, Pinda aliwaambia wabunge kwamba hali ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini kwa ujumla, imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi, kutokana na mavuno mazuri katika msimu wa kilimo wa 2013/2014.
Kuhusu mwenendo wa malipo ya madeni ya ununuzi wa mahindi kwa msimu wa 2014/2015, Pinda alisema hadi kufikia Desemba 2014 Serikali ilikuwa inadaiwa Sh bilioni 89 na wakulima waliouuzia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) mahindi.   
Hadi kufikia Januari 29 mwaka huu, kwa mujibu wa Waziri Mkuu,  Serikali ilikuwa imelipa wakulima hao Sh bilioni 15 na kubakiza deni la Sh bilioni 74. 
Alisema katika juhudi za Serikali za kutatua changamoto ya deni hilo,  mwezi huu inatarajia kulipa Sh bilioni 40 na kubakia na deni la Sh bilioni 34 ambazo zitalipwa kutokana na mkopo wa benki ya CRDB wa Sh bilioni 15 na Bajeti ya Serikali.

No comments: