Mshindi wa Sh milioni 10
katika shindano la wazo bora la biashara linaloendeshwa na Mwenyekiti wa
Makampuni ya IPP Media, Reginald Mengi kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa
twitter ametangazwa na wengine kumi wamejinyakulia kitita cha Sh milioni moja.
Fredrick Shayo, mhitimu wa chuo kikuu na mjasiriamali
anayejishughulisha na ufugaji wa kuku wa kienyeji ndiye aliyetangazwa kuwa
mshindi kati ya washiriki 1,680 waliotuma maombi yao na kuingia katika kinyang'anyiro
hicho cha kuwania Sh milioni 10 kama
mtaji wa kuendeleza wazo bora la biashara.
Akizungumza katika hafla fupi
ya kumtangaza mshindi wa shindano hilo, Dk Mengi aliwaasa vijana kutochagua
kazi kwani kila kazi ina malipo.
“Vijana wengi ambao hawana
kazi wanachagua kazi. Kila mtu anatakiwa afanye kazi ilimradi inampatia
mshahara na baada ya hapo utakuwa na mtaji wa kujiendeleza katika shughuli
nyingine na hata kufungua kampuni,” alisema
Mengi.
Alisema wapo Watanzania
wanaowakatisha tamaa wengine kwa kusema Watanzania hawawezi kuwa mamilionea.
Kitu ambacho si kweli kwani kuwa na mali nyingi kunatokana na juhudi ya kazi na
pia ni baraka kutoka kwa Mungu.
“Mimi nawashangaa sana baadhi
ya watu wanaosema hakuna mtu anaweza kuwa milionea hapa Tanzania. Kwa maana
hiyo wanasubiri mamilionea kutoka nje ya nchi ili waweze kuwapigia magoti. Hii
ni kuwakatisha tamaa vijana wenye ari ya kujituma na kutaka kuwa matajiri,”
alisema.
Kwa upande wa mshindi wa
shindano hilo Shayo alisema amefurahi sana kushinda kiasi hicho cha pesa kwani
kitamsaidia kuongeza uzalishaji wa kuku wa kienyeji na kuuza katika maeneo
mengi na kuwasaidia wengine kuongeza ufugaji wa kuku.
Washindi wengine walioingia
kumi bora walizawadiwa kila mmoja Sh
milioni moja kama pongezi ya kuwa
wabunifu na kuwatia moyo wasikate tamaa na shughuli zao za ujasiriamali
wanazozifanya.
No comments:
Post a Comment