MNADHIMU WA CCM BARAZA LA WAWAKILISHI AZIKWA


Mamia ya wananchi wakiongozwa na Rais wa Zanzibar,  Dk Ali Mohamed Shein walihudhuria maziko ya aliyekuwa mnadhimu wa Chama Cha Mapinduzi Baraza la Wawakilishi na Mwakilishi wa jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin kijijini kwao Kiungoni Makunduchi mkoa wa kusini Unguja.

Awadh alifariki ghafla juzi wakati alipokuwa katika ofisi kuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa ambapo alikuwa akihudhuria vikao mbalimbali vya Chama Cha Mapinduzi.
Mwili wa marehemu Awadh uliagwa na viongozi mbalimbali wa serikali  na vyama vya siasa wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Akitoa salamu kwa waombelezaji waliohudhuria msiba huo katika jengo la Baraza la Wawakilishi, shehe kutoka Kamisheni ya Wakfu na mali za amana, Thabit Norman Jongo alisema ni msiba mkubwa kwa taifa na familia ya marehemu kwa ujumla.
Hata hivyo, alisema msiba huo unawakumbusha waumini na wananchi kwamba kila nafsi itaonja umauti, kwa hiyo njia pekee ya kujiweka salama katika safari ya mwisho, kwa kila binadamu ni kufanya ibada.
Mwili wa marehemu Awadh uliswaliwa katika Msikiti wa Masjid Noor ambapo safari ya mwisho ya marehemu ilianzia hadi Makunduchi kilomita 54 kutoka mjini.

No comments: