MARUFUKU KUVUA KASA ENEO LA ZANZIBAR


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema ni marufuku kwa wavuvi kuvua samaki aina ya kasa katika eneo la bahari ya Zanzibar ambapo viumbe hao wapo katika hatari ya kutoweka duniani.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdilahi Jihadi Hassan alisema licha ya Serikali kupiga marufuku uvuvi wa kasa, bado wavuvi wamekuwa wakiendesha uvuvi huo kwa kutumia mitego ambayo pia imepigwa marufuku.
Jihadi alisema hayo huko Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja wakati aliposhiriki katika zoezi la kuwaachia huru jumla ya kasa 33 kurudi baharini na kuanza maisha ya kudumu.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inasisitiza kwamba uvuvi wa kasa ni marufuku kwa mujibu wa sheria za kimataifa kwa sababu viumbe hao wapo katika hatari ya kutoweka duniani kutokana na mazingira mbalimbali ikiwemo kasi ya uvuvi wake,” alisema.
Ofisa Mwandamizi wa kituo kinachohifadhi kasa huko Nungwi, Fakih alisema katika kipindi cha miaka minne sasa zaidi ya kasa 300 wameachiwa huru kuishi maisha ya kudumu baharini.
Alisema wamekuwa wakihifadhi kasa hapo katika njia mbalimbali ikiwemo wale kasa wanaohifadhiwa hapo wakitotoa mayai yao na kuhifadhiwa kwa muda wa miaka mitatu na baadaye kuachiwa.
“Kituo chetu miongoni mwa kazi zake kubwa ni kuhifadhi kasa katika hatua za awali ikiwemo mayai hadi yanapototolewa na kuwahifadhi hadi wanapokuwa wakubwa na kuwarudisha baharini,” alisema.
Baadhi ya wavuvi wanadaiwa kuendelea kuvua kasa kinyume na sheria ambapo nyama yake kutengenezwa wakati wanapokuwa baharini ili kuogopa kuchukuliwa hatua za kisheria na maofisa wa uvuvi.
Ofisa mmoja wa Idara ya Uvuvi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ali Issa alikiri kuwepo kwa kasi ya uvuvi haramu wa kasa ambapo wavuvi hutumia nyavu kwa ajili ya kuwanasa.
“Tatizo la uvuvi haramu wa kasa bado lipo ambapo wavuvi hutumia mitego ya nyavu za kunasa samaki hao nyakati za usiku,” alisema.
Baadhi ya maofisa wa mazingira kutoka idara ya uvuvi wamefafanua kwamba kasa hivi sasa wamepungua kasi ya kutaga katika maeneo ya fukwe za bahari kutokana na ujenzi wa mahoteli ya kitalii zinazofanywa karibu na fukwe hizo.
“Kasa wamepungua kutaga katika maeneo mengi ya fukwe ziliopo Zanzibar kwa sababu ya kuogopa kukamatwa na watu wanaotembea karibu na fukwe,” alisema.
Alisema kwa kawaida kasa anapotaka kutaga mayai hulazimika kuja nchi kavu pembezoni mwa fukwe ambapo huhitaji utulivu huku akichimba mashimo tofauti na kutaga na baadaye kurudi baharini.

No comments: