MADEREVA WA UDA WAPINGA UTARATIBU WA KUWAACHISHA KAZIMadereva wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) wamelalamikia shirika hilo kuwapunguza kazini hivi karibuni bila kufuata utaratibu unaofaa, ikiwa ni pamoja na mchanganuo wa malipo yao.

Wakizungumza na mwandishi jana, madereva hao walilalamikia shirika hilo kuvunja mkataba waliowekeana na kampuni hiyo ambao ni wa miaka miwili na kuamua kutafuta sababu za kuwasimamisha kazi.
Baadhi ya madereva walikuwepo katika ofisi za UDA zilizoko Kamata, Ilala walisema wameshangazwa  na shirika hilo kuwatafutia sababu wafanyakazi za kuwafukuza kazi na kupuuza haki zao.
“Awali tulikuwa tukifanya kazi kwa utaratibu wa dereva wawili kwa gari moja ambapo leo ukiwa kazini kesho yake unapumzika na mwenzako anaingia kazini, lakini ghafla tulibadilishiwa utaratibu mwezi huu ikawa kila gari dereva ni mmoja tu ambaye anatakiwa kufanya kazi siku tano mfululizo,” alisema Simon Kamwela.
Alisema hata hivyo walipewa fomu ambazo ni za hiari za kusaini ambayo zimeshajazwa zilizokuwa zinawataka kukubali mfumo huo wa kuendesha gari siku tano mfululizo katika wiki na pia kukiri kupeleka mapato ya kampuni kama dereva alivyopangiwa kila siku.
Madereva hao wanadai kuwa baada ya kufukuzwa kazi barua wamepewa kuanzia Februari 10 mwaka huu na wengine wanaendelea kupewa mpaka sasa wakati barua zinaeleza kuwa wamepunguzwa kazi toka Februari 9 mwaka huu.
Paulo alisema mshahara pia wa mwezi wa kwanza ambao wameufanyia kazi hawajalipwa aidha alisema wameenda katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuangalia michango yao lakini wameambiwa hakuna michango iliyowasilishwa.
Msemaji wa UDA, George Maziku alisema ni kweli Shirika la UDA liko katika kupunguza wafanyakazi wake wale ambao hawafikii malengo waliyowekewa ambapo kwa upande wa madereva ni Sh 300,000 kwa siku kwa magari ya Mnazi Mmoja Feri na Sh 205,000 kwa ruti nyingine.
“Madereva wote wanajua kabisa na kwenye mikataba yao wamesaini kukusanya fedha hizo kwa siku, wasiotimiza tunawaandikia deni lakini wale ambao madeni yao yamekuwa makubwa pamoja na makosa mengine ya kinidhamu shirika limeamua kuwapunguza,” alisema Maziku.

No comments: