Maandalizi hafifu ya watahiniwa wa mitihani
kwa ngazi zote ndio chanzo kikubwa cha kuwapo udanganyifu katika mitihani ya
mwisho.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Idara ya Fedha
na Utawala wa Baraza la Mitihani ya Tanzania (Necta), Daniel Mafie aliyekuwa
akizungumzia mafanikio ya baraza hilo kwa niaba ya Katibu Mtendaji.
Alisema pamoja na kupungua kwa watahiniwa
wanaofanya udanganyifu kwenye mitihani, lakini maandalizi hafifu ya wanafunzi
wanachangia tatizo hilo.
“Unakuta mtahiniwa hajajiandaa vizuri na hapo
hapo anataka kuwa na matokeo mazuri, hilo ndilo linalowafanya kuingia katika
udanganyifu. Jamii inatakiwa kujua njia pekee ya kufanya vizuri katika mitihani
ya mwisho ni kuwa na maandalizi mazuri,” alisema.
Alisema, Baraza lake kwa kushirikiana na
Kamati za Uendeshaji wa Mitihani katika ngazi za Mikoa na Wilaya na wasimamizi wameweza kudhibiti tatizo la
wizi wa mitihani kwa kiasi kikubwa.
Alitolea mfano mtihani wa kumaliza elimu ya
msingi, udanganyifu umepungua kutoka watahiniwa 9,736 wa mwaka 2011 hadi
mtahiniwa mmoja mwaka 2014, wakati Kidato cha Nne ni watahiniwa 3,303 kwa mwaka
2011 hadi watahiniwa 184 kwa mwaka 2014.
Katika matokeo ya mwaka 2014 yaliyotangazwa
hivi karibuni kati ya watahiniwa 184 ambao matokeo yao yalifutwa kwa
udanyanyifu, watahiniwa 128 walikuwa ni watahiniwa wa kujitegemea katika vituo
viwili na watahiniwa 56 wakiwa ni watahiniwa wa shule.
Kwa upande wa Kidato cha Sita udanyanyifu
umepungua kutoka watahiniwa 11 kwa mwaka 2011 hadi watahiniwa watatu mwaka
2014.
No comments:
Post a Comment