Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekiruhusu
kiwanda cha U-Fresh Food Limited cha Tegeta, Dar es Salaam, kiendelee kuzalisha
juisi ya U-Fresh, kwa kuwa kimetimiza masharti ya viwango vya ubora vya juisi
hiyo.
Mdhibiti Viwango vya Ubora wa bidhaa wa shirika
hilo, Editha Protace alisema wakati wa kukifungua kiwanda hicho juzi kuwa,
baada ya kukifanyia ukaguzi upya na kupima sampuli za juisi itakayoanza
kuzalishwa, TBS imeridhishwa na maboresho muhimu yaliyofanyika.
"Pamoja na kuchukua vipimo muhimu na
kuvifanyia uchunguzi kwenye maabara yetu ya chakula, tumeona kuna tofauti kubwa
na vigezo vya viwango vya ubora katika juisi hiyo vimezingatiwa. Sasa walaji
wanaweza kuanza kuitumia kwa sababu ni salama," Protace alisema.
Akifafanua alisema, vipimo vimeonesha kuwa
sukari tamu iliyokuwa ikitumiwa awali haijatumika tena.
"Cha msingi ni wanywaji kuwa makini na
tarehe ya kutengenezwa kwa juisi hiyo kuepuka kupata iliyozuiwa awali, endapo
kutakuwa na wafanyabiashara waliofanikiwa kuzificha hata baada ya msako".
Anasisitiza kuwa, juisi yoyote itakayoonesha
imetengenezwa kabla ya Februari 16, mwaka huu, itakuwa miongoni mwa zilizozuiwa
zisiuzwe awali, hivyo, atakayeinunua airejeshe kiwandani hapo au TBS kwa ajili
ya ufuatiliaji zaidi.
Meneja
Masoko wa kiwanda hicho, Kephas Gembe aliwaahidi watanzania kuwa watazalisha
juisi hizo kwa kuzingatia viwango vilivyopitishwa na shirika hilo, kulinda afya
za walaji na mazingira.
Kwa mujibu wake, hakuna kiungo kisichofaa
kitakachotumika kutengeneza juisi hiyo, hivyo wanapoinywa wawe na amani.
"Tunaomba watakaoona juisi za zamani zikiendelea kuuzwa watutaarifu au
kuijulisha TBS kwa hatua zaidi.
Miongoni mwa maboresho yaliyofanywa kiwandani
hapo ni pamoja na kuweka mazingira ya kiwanda hicho katika hali ya usafi,
kuandika maandishi katika ukuta wake kuwa ni kiwanda kinachozalisha juisi hiyo
pamoja na kuweka maelezo muhimu katika vifungashio ikiwemo viungo vilivyotumika
na anuani ya mzalishaji.
No comments:
Post a Comment