KIJIJI CHAUNGANISHWA NA UMEME WA KUTUMIA KUNI


Wakazi wa kijiji cha  Uchindile wilayani Ifakara mkoani Morogoro wamepata umeme unaozalishwa kwa kutumia kuni baada ya kuzinduliwa kwa mtambo wa 10kW uliotolewa na kampuni ya kimataifa ya Camco Clean Energy.

Mtambo huo wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 75 ulizinduliwa na Mwakilishi wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), Rogness Swai katika hafla iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, wakiwemo wananchi wa kijiji hicho.  
Pamoja na Camco Clean Energy Tanzania iliyofadhiliwa na USAID ili kufanikisha mradi huo utakaokabidhiwa kwa serikali ya kijiji hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo nchini, Jeff Felten aliwataja wengine waliochangia ujenzi wake kuwa ni kampuni ya Village Industrial Power (VIP) na Kiwanda cha Karatasi cha Mufindi (MPM) cha Mgololo, wilayani Mufindi.
Felten alisema mtambo huo utawezesha kaya 100 kati ya 265 za kijiji hicho kilichopo zaidi ya kilomita 100 toka Mafinga, wilayani Mufindi mkoani Iringa kuwa za kwanza nchini kunufaika na nishati hiyo inayotarajiwa pia kuzinduliwa mkoani Kigoma hivi karibuni.

No comments: