JKT YAWASUTA WAHITIMU WANAOTAKA KUANDAMANA


Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewataka vijana waliomaliza katika jeshi hilo, kutambua kuwa walikula kiapo cha utii wakati wa kuhitimu mafunzo, hivyo suala la kuandamana ni kinyume na kiapo chao.

Vijana hao waliotumikia Jeshi la Kujenga Taifa Operesheni za nyuma na kumaliza mkataba wa miaka miwili,  wameambiwa shinikizo lao la kulazimisha ajira kwa kuandamana ni kinyume cha sheria za nchi.
Taarifa kwa vyombo vya habari, iliyotolewa na Makao Makuu ya  jeshi hilo, jijini Dar es Salaam jana, ilisema kipengele kimoja cha masharti ya kujiunga na JKT kinasema baada ya mkataba, wanapaswa kurejea nyumbani na hawapaswi kudai jeshi liwatafutie ajira.
Ilieleza kwamba masharti ya jeshi hilo, huwekwa bayana kwa vijana wanapojiunga na JKT. Vijana hao wanatakiwa  kujua masharti  hayo na taratibu  za  JKT na kuelewa kuwa JKT halitoi ajira.
Taarifa hiyo ilinukuu kipengele kimojawapo cha masharti, kinachosema “Kwa kipindi chote nitakachokuwa ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa nitakuwa nafanya mafunzo ya kijeshi na ya stadi za kazi na maisha, na baada ya mkataba nitarejea nyumbani. Hivyo sitalidai Jeshi la Kujenga Taifa ajira, wala kulitaka linitafutie ajira/kazi”.
Ufafanuzi huo ulitolewa, kutokana na vijana zaidi ya 200 waliohitimu mafunzo ya JKT kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2013, kutangaza hivi karibuni kuwa wataandamana wiki ijayo kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete, kumweleza shida zao, ikiwemo kutokuwa na ajira tangu wamalize mafunzo.
Jeshi hilo lilisema ni vema vijana hao, wakatambua kuwa tatizo la ajira siyo kwao peke yao, ni tatizo la ulimwengu mzima Tanzania, ikiwemo hivyo wanashauriwa kutumia stadi za kazi kujiajiri wenyewe.
“Kutokana na dhumuni la kuundwa JKT  Taifa, halina dhamana ya kuajiri bali kufunza vijana wa taifa hili umoja, stadi za kazi na uzalendo baada ya hapo wawe wenye sifa za kuajiriwa hupata ajira katika taasisi mbalimbali za serikari na binafsi,” ilisema taarifa hiyo.
Hata hivyo, jeshi hilo limesema tangu  mwaka 2003 hadi 2014,  vijana 24,708 wameajiriwa katika vyombo  vya ulinzi na usalama. Kati ya hao, vijana 21,977 wakiwemo wavulana 17,307 na wasichana 4,670,  wameajiriwa na Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kwa upande wa  Polisi,  vijana 3,965  wameajiriwa ambao kati yao, wavulana ni 2,943;  Magereza  wameajiriwa 2,139 kati yao wavulana ni 2,044; Zimamoto vijana 100 wavulana wakiwa  78 na taasisi zingine wameajiriwa vijana 592
Aidha, alisema vijana 1,622 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali kamavile  migodi ya dhahabu ya Geita, Mamlaka ya Bandari na Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa).
 Taarifa hiyo ilisema JKT  ilianzishwa Julai 10, 1963 kwa lengo la kuwaweka pamoja vijana na kuwapa malezi, kuhusu uzalendo na umoja ili kuondoa dalili za matabaka, zilizoanza kujitokeza katika jamii baada ya uhuru.
Serikali ilirejesha mafunzo ya jeshi hilo kwa vijana wa kujitolea mwaka 2001 baada ya kusitishwa mwaka 1994.
Alisema  masharti ya kujiunga na jeshi hilo kwa vijana wa kujitolea ni kuhakikisha wahusika wanafahamu masharti na  taratibu, ikiwemo kuelewa kwamba  JKT haitoi ajira.
Takwimu zinaonesha kuwa tangu kurejeshwa kwa mafunzo ya JKT mwaka 2001 hadi mwaka jana, vijana 104,594 wamejiunga na JKT wakiwemo wavulana 76,832 na wasichana 27,762.

No comments: