Tatizo
la kukatika kwa umeme katika Jiji la Dar es Salaam litakwisha baada ya Serikali
ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la JICA kutoa msaada wa zaidi
ya Sh
bilioni 66, kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa vituo vipya vya kupozea
umeme jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felchesmi Mramba alisema alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari,
Makao Makuu ya Tanesco Dar es Salaam.
Mramba
alisema mradi huo utakapokamilika utapunguza mzigo kwenye vituo vya Oysterbay,
Mbezi Beach na Makumbusho hivyo kuondoa adha ya kukatika kwa umeme kutokana na
kuzidiwa.
“Vile
vile wananchi wanaoishi maeneo jirani na vituo vipya watapata umeme wa uhakika
na ulio bora zaidi. Kituo cha kupozea umeme cha Ilala kitaongezewa transfoma
mbili hivyo kuweza kutoa umeme mwingi zaidi kwenye maeneo ya katikati ya Jiji
pamoja na Kariakoo,” alisema.
Mkurugenzi
huyo alisema kuwa, Kituo cha Muhimbili kitakuwa na laini ya peke yake
itakayopeleka umeme kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili hivyo kuwa na umeme wa
uhakika.
Mramba
alisema Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na ya Japan walikubaliana
kukarabati miundombinu ya umeme kwa kupanua na kujenga vituo vipya vya kupozea
umeme katika Jiji la Dar es Saalam.
Alitaja
kazi zitakazofanyika katika mradi huo kuwa ni ukarabati wa kituo cha kupozea
umeme cha Ilala kwa kuweka transfoma mpya mbili za ukubwa wa MVA 60,kV 132/33.
Vile
vile ujenzi wa jengo jipya la ‘control’ katika kituo cha kupoozea umeme cha Ilala,
uwekaji na uvutaji wa waya wa njia ya pili ya kusafirisha umeme ya msongo wa
kilovoti 132 kutoka Ubungo hadi Ilala na kupanua kituo cha kupozea umeme cha
Msasani 33/11kV kwa kuweka transfoma nyingine mpya ya MVA 15, Kv 33/11.
No comments:
Post a Comment