Rais
Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya kwa kutengua
uteuzi wa wakuu wa wilaya 12, kuteua wapya 27 na wengine 64 kubadilishwa vituo
vyao.
Wakuu wa wilaya 42 ndiyo pekee wameendelea
kubaki katika vituo vyao vya kazi.
Mabadiliko hayo yalitangazwa mjini Dodoma
jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
yakizingatia nafasi za wazi 27 zilizotokana na kufariki dunia kwa wakuu wa
wilaya watatu, kupandishwa cheo watano kuwa wakuu wa mikoa na kupangiwa
majukumu mengine wakuu wa wilaya 7.
Mabadiliko hayo yameibua baadhi ya majina
muhimu katika siasa nchini, kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu na wakati huo
huo yamekidhi madai ya wanasiasa, waliokuwa wameshikia bango kwamba uteuzi wa
baadhi ya wakuu wa wilaya utenguliwe.
Baadhi ya majina mapya ni pamoja na Paul
Makonda, Frederick Mwakalebela na Mboni Mhita.
Paul
Makonda
Hii ni moja ya sura mpya, zilizoibuliwa
kupitia mabadiliko hayo. Makonda anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar
es Salaam. Makonda ni Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa Umoja wa
Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM). Ni
miongoni mwa vijana maarufu katika siasa ndani ya CCM na nchini kwa ujumla.
Kijana huyu amejipambanua katika suala zima la
kambi za kuwania urais, baada ya kujitokeza hadharani kuzungumzia mbio za
urais, akishutumu baadhi ya watu kwamba wanavuruga chama kwa lengo la kutaka
urais 2015.
Aliungwa mkono na baadhi ya wakongwe wa chama hicho, ambao walimsifu kwamba ni kijana jasiri kwa kukemea vitendo vinavyofanywa na baadhi
ya wanaowania nafasi hiyo na kusema kwa kufanya hivyo, chama kitaendelea
kupendwa.
Aidha katika mchakato wa Katiba Mpya, Makonda
ni miongoni mwa vijana waliotengeneza majina kuanzia kwenye Bunge Maalumu la
Katiba hadi nje ya bunge hilo.
Alikuwa miongoni mwa wanasiasa, waliosimama
kidete kupigia debe muundo wa Muungano wa Serikali mbili, uliopitishwa ndani ya
Katiba Inayopendekezwa.
Katika Bunge hilo Maalumu mjini Dodoma, Makonda alikuwa miongoni mwa
wajumbe waliopanda hadharani baadhi ya vipengele vilivyowasilishwa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na
Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Ni katika bunge hilo, kwa kuzingatia msimamo wake, Makonda
alijikuta akisigana na mjumbe mwingine, Ezekiel Oluoch aliyekuwa akipinga mabadiliko ya Kanuni,
yaliyotoa nafasi kwa wajumbe kupiga kura wakiwa nje ya Bunge. Kanuni hiyo, hata
hivyo, ilipitishwa.
Oluoch aliwasilisha malalamiko kwa Katibu wa
Bunge Maalumu la Katiba, Yahya Hamad, akisema Makonda alisema uongo juu yake
kwa kusema anataka kugombea nafasi ya ubunge huku akimtaka asitumie Bunge
Maalumu la Katiba kujitangaza.
Jina la Makonda liliendelea kusikika pia
Novemba mwaka jana, alipotuhumiwa kuhusika katika vurugu zilizotokea jijini Dar
es Salaam kwenye mdahalo ulioitishwa na Mfuko wa Mwalimu Nyerere kujadili
Mchakato wa Katiba pamoja na Katiba Inayopendekezwa.
Vurugu hizo zilihusisha kundi la vijana,
waliodaiwa kumzomea Jaji Warioba,
alipokuwa akiwasilisha mada katika mdahalo huo.
Hata hivyo, Makonda alikanusha kuhusika
kumdhalilisha Warioba; akisema wamelenga kumchafua kisiasa. Alijitetea
kwamba ndiye alisaidiana na watu
wengine, kumtoa nje ya ukumbi mzee huyo asidhuriwe na vijana, waliokuwa
wakifanya vurugu, ikiwemo kurusha chupa za maji.
Frederick
Mwakalebela
Mwakalebela amepangiwa wilaya ya Wanging'ombe
mkoani Njombe. Zinapotajwa siasa za mkoa
wa Iringa na hata utwaaji wa Jimbo la Iringa Mjini kwa upinzani, jina la
Mwakalebela linahusishwa.
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 uliompa
ushindi Mchungaji Peter Msigwa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) katika Jimbo la Iringa Mjini,
kulikuwa na kauli za kushutumu kitendo cha Mwakalebela kuenguliwa katika kura
za maoni za CCM.
Wachambuzi wa mambo ya siasa wanaeleza kuwa
kitendo cha Mwakalebela kupewa Wilaya ya Wanging'ombe ambayo
ipo jirani na Iringa Mjini, kutampa
fursa ya kujijenga zaidi kisiasa na hivyo wakati utakapofika atatimiza tena
azma yake ya kuwa mwakilishi wa Iringa Mjini.
Umaarufu wa Mwakalebela ulianzia wakati akiwa
Katibu Mkuu wa lililokuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Alishikilia nafasi hiyo kuanzia mwaka 2006
hadi 2010.
Baada ya mkataba wake kumalizika, Mwakalebela
alijitosa kuomba kugombea ubunge wa Iringa Mjini kupitia CCM. Hata hivyo,
alienguliwa na chama kugombea nafasi
hiyo licha ya kuwa alikuwa ameshinda kwenye kura za maoni.
Badala yake,
CCM ilimteua Monica Mbega
aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mkuu wa Mkoa, kuingia kwenye
kinyang'anyiro hicho. Hata hivyo, Mbega alidondoshwa na Mchungaji Msigwa.
Waliotenguliwa
Ingawa haikuwekwa bayana sababu za baadhi
kutenguliwa ukuu wa wilaya na wengine kuwekwa ‘kiporo’ kwa ajili ya kupangiwa
majukumu mengine, inadhihirisha uteuzi
huu umejaribu pia kuzingatia madai na malalamiko dhidi ya baadhi ya wakuu wa
wilaya.
Baadhi yao, wameponzwa na migogoro kati ya
wakulima na wafugaji. Mfano ni Martha
Umbulla aliyekuwa Wilaya ya Kiteto.
Katika mkutano wa Bunge, Mei mwaka jana,
Umbulla alishikiwa bango na wabunge kadhaa waliotaka uteuzi wake wa ukuu wa
wilaya utenguliwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ndiyo chanzo cha migogoro,
iliyosababisha mauaji ya wakulima kutoka wilayani Kongwa yaliyofanyika wilayani
kwake, Kiteto.
Mathalani,
Mbunge wa Arusha, Godbless Lema alimshutumu Umbulla (Mbunge wa Viti
Maalum) kwamba alikuwa akiwabagua wananchi.
Ingawa Umbulla
alijaribu kueleza kilichojiri, pia
Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai ambaye ni Naibu Spika wa Bunge, alimshutumu
Umbulla akisema ubaguzi wa viongozi wilayani Kiteto ndicho chanzo cha mauaji
hayo.
Waliowekwa
kiporo
Miongoni mwa ambao Waziri Mkuu amesema kuwa
watapangiwa majukumu mengine ni Mrisho Gambo, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya
Korogwe ambaye mwaka jana, alifikishwa mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi
wa Umma jijini Dar es Salaam,
akituhumiwa kutumia vibaya madaraka
yake.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Anna Mwalende ni miongoni
mwa waliofika mbele ya Baraza kutoa ushahidi dhidi ya Gambo na kueleza namna
alivyodhalilishwa na kunyanyaswa .
Mbele ya Mwenyekiti wa Baraza, Jaji mstaafu
Hamisi Msumi, shahidi huyo alidai mkuu huyo wa wilaya amekuwa na lugha chafu kwa viongozi wenzake,
ana utawala wa mabavu bila kuzingatia kanuni na sheria, jambo ambalo ni kikwazo
kwa maendeleo ya wilaya hiyo.
Mabadiliko yenyewe:
Walioenguliwa
Wakuu wa wilaya ambao uteuzi wao umetenguliwa
na vituo vyao katika mabano ni James Ole
Millya (Longido), Elias Wawa Lali (Ngorongoro), Alfred Msovella (Kongwa), Danny
Makanga (Kasulu), Fatma Kimario (Kisarawe), Elibariki Kingu (Igunga), Dk
Leticia Warioba (Iringa), Evarista Kalalu (Mufindi) ,Abihudi Saideya (Momba),
Martha Umbulla (Kiteto), Khalid Mandia (Babati) na Elias
Goroi (Rorya).
Wanaopangiwa
majukumu mengine
Cosmas Kayombo (Simanjiro), Ngemela Lubinga,
(Mlele), Juma Madaha, (Ludewa), Mercy Silla, (Mkuranga), Ahmed Kipozi
(Bagamoyo), Mrisho Gambo (Korogwe)
na Elinas Pallangyo (Rombo).
Wakuu
wa Wilaya Wapya
Zelothe Steven aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Mtwara ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya (Musoma), Mboni Muhita ambaye
ni Makamu Mwenyekiti wa Taifa Umoja wa Vijana wa CCM, anakuwa Mkuu wa Wilaya ya
Mufindi.
Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa kitengo
cha hamasa cha Umoja wa Vijana wa Chama
Cha Mapinduzi (UVCCM), Paul Makonda anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,
Shaabani Kissu ambaye ni mtangazaji wa Shirika
la Utangazaji la Taifa (TBC), anakuwa mkuu wa Wilaya ya Kondoa.
Wengine ni Mariam Mtima (Ruangwa), Dk Jasmini
Tiisike (Mpwapwa), Paloleti Mgema (Nachingwea), Fadhili Nkurlu, (Misenyi),
Felix Lyaniva (Rorya), Fredrick Mwakalebela (Wanging'ombe), Fransis Mwango
(Bahi), Kimiang'ombe Samwel (Kiteto).
Wengine ni Husna Msangi (Handeni), Emmanuel
Uhaula (Tandahimba), Hashim Mngandilwa (Ngorongoro), Mariam Juma (Lushoto),
Thea Ntara (Kyela), Ahmad Nammohe (Mbozi), Pili Moshi (Kwimba), Mahmoud Kambona
(Simanjiro), Glorius Luoga (Tarime), Zainabu Telack (Sengerema), Zuhura Ally
(Uyui).
Waliobadilisha
vituo
Nyerembe Munasa anatoka Arumeru kwenda Mbeya, Jordan Rugimbana kutoka
Kinondoni kwenda Morogoro, Fatma Ally
kutoka Chamwino kwenda Mtwara, Lephy Gembe kutoka Dodoma Mjini kwenda
Kilombero, Christopher Kangoye kutoka Mpwapwa kwenda Arusha, Omary Kwaang’
kutoka Kondoa kwenda Karatu, Francis Isack kutoka Chemba kwenda Muleba na Betty Mkwasa kutoka Bahi kwenda Dodoma Mjini.
Wengine ni Agnes Hokororo kutoka Ruangwa
kwenda Namtumbo, Regina Chonjo kutoka Nachingwea kwenda Pangani, Husna Mwilima
kutoka Mbogwe kwenda Arumeru, Gerald Guninita kutoka Kilolo kwenda Kasulu,
Zipporah Pangani kutoka Bukoba kwenda Igunga na Issa Njiku kutoka Misenyi
kwenda Mlelea.
Richard Mbeho kutoka Biharamulo kwenda Momba,
Lembris Marangushi kutoka Muleba kwenda Rombo, Ramadhani Maneno kutoka Kigoma
kwenda Chemba, Venance Mwamoto kutoka Kibondo kwenda Kaliua, Gishuli Charles
kutoka Buhigwe kwenda Ikungi.
Wengine ni Novatus Makunga kutoka Hai kwenda
Moshi, Anatory Choya kutoka Mbulu kwenda Ludewa, Christine Mndeme kutoka Hanang kwenda Ulanga, Jackson
Musome kutoka Musoma kwenda Bukoba, John Henjewele kutoka Tarime kwenda
Kilosa, Dk Norman Sigalla kutoka Mbeya
kwenda Songea, Dk Michael Kadeghe kutoka
Mbozi kwenda Mbulu, Crispin Meela kutoka Rungwe kwenda Babati, Magreth Malenga
kutoka Kyela kwenda Nyasa.
Wengine ni Saidi Amanzi kutoka Morogoro kwenda
Singida, Antony Mtaka utoka Mvomero kwenda Hai, Elias Tarimo kutoka Kilosa
kwenda Biharamulo, Francis Miti kutoka Ulanga kwenda Hanang, Hassan Masala
kutoka Kilombero kwenda Kibondo.
Angelina Mabula anatoka Butiama kwenda Iringa, Farida Mgomi kutoka
Masasi kwenda Chamwino, William Ndile kutoka Mtwara kwenda Kalambo, Ponsian
Nyami kutoka Tandahimba kwenda Bariadi, Mariam Lugaila kutoka Misungwi kwenda
Mbongwe, Mary Onesmo kutoka Ukerewe kwenda Buhigwe, Karen Yunus kutoka
Sengerema kwenda Magu, Josephine Matiro kutoka Makete kwenda Shinyanga, Joseph
Mkirikiti kutoka Songea kwenda Ukerewe.
Wengine ni Abdula Lutavi kutoka Namtumbo
kwenda Tanga, Ernest Kahindi kutoka Nyasa kwenda Longido, Anna Nyamubi kutoka
Shinyanga kwenda Butiama, Rosemary Kirigini kutoka Meatu kwenda Maswa, Abdallah
Kihato kutoka Maswa kwenda Mkuranga, Erasto Sima kutoka Bariadi kwenda Meatu,
Queen Mulozi kutoka Singida kwenda Urambo, Yahya Nawanda kutoka Iramba kwenda
Lindi, Manju Msambya kutoka Ikungi kwenda Ilemela, Saveli Maketta kutoka Kaliua
kwenda Kigoma, Bituni Msangi kutoka Nzega kwenda Kongwa na Lucy Mayenga kutoka
Uyui kwenda Iramba.
Wengine waliohamishwa ni Majid Mwanga kutoka
Lushoto kwenda Bagamoyo, Muhingo Rweyemamu kutoka Handeni kwenda Makete, Hafsa
Mtasiwa kutoka Pangani kwenda Korogwe, Dk Nassoro Hamid kutoka Lindi kwenda
Mafia, Festo Kiswaga kutoka Nanyumbu kwenda Mvomero, Selemani Mzee kutoka
Kwimba kwenda Kilolo, Esterina Kilasi kutoka Wanging’ombe kwenda Muheza, Subira
Mgalu kutoka Muheza kwenda Kisarawe na Jacqueline Liana kutoka Magu kwenda
Nzega.
Waliobaki
Vituoni
Waziri Mkuu alitaja waliobaki kwenye vituo
vyao ni Jokwika Kasunga (Monduli), Raymond Mushi (Ilala), Sophia Mjema
(Temeke), Amani Mwenegoha (Bukombe), Ibrahim Marwa (Nyang'hwale), Rodrick
Mpogolo (Chato), Manzie Mangochie (Geita), Darry Rwegasira (Karagwe) na
Benedict Kitenga (Kyerwa).
Wengine ni Constantine Kanyasu(Ngara),
Paza Mwamulima(Mpanda), Peter Kiroya
(Kakonko), Hadija Nyembo(Uvinza), Dk Charles Mlingwa(Siha), Shaibu
Ndemanga (Mwanga), Herman Kapufi (Same),
Ephraim Mbaga (Liwale), Abdallah Ulega (Kilwa) na Joshua Mirumbe.
Aliwataja wengine ni Deodatus Kinawiro
(Chunya), Rosemary Senyamule (Ileje), Gulamhusein Shaban (Mbarali), Christopher
Magala (Newala), Baraka Konisaga(Nyamagana), Sarah Dumba (Njombe), Halima
Kihemba (Kibaha), Nurdin Babu (Rufiji), Mathew Sedoyeka (Sumbawanga).
Iddi
Kimanta (Nkasi), Chande Nalicho (Tunduru), Senyi Ngaga (Mbinga), Wilson Nkambaku (Kishapu),
Benson Mpesya (Kahama), Paul Mzindakaya (Busega), Georgina Bundala (Itilima),
Fatma Toufiq (Manyoni), Edward Ole Lenga (Mkalama), Hanifa Selengu (Sikonge),
Suleiman Kumchaya (Tabora), Mboni Mgaza (Mkinga) na Selemani Liwowa (Kilindi).
No comments:
Post a Comment