EL MERREIKH YAIFUNGASHA VIRAGO AZAM, KMKM NAYO NJE


Safari ya timu ya soka ya Azam FC kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika imefikia kikomo baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-0 mbele ya vijana wa El Merreikh ya Sudan katika mechi iliyomalizika muda mfupi uliopita mjini Khartoum.

Katika mechi hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa Azam walicheza kwa kujihami zaidi, hadi mapumziko El Merreikh walitoka vifua mbele kwa 1-0.
Kipindi cha pili mambo yakawawia vigumu mno Azam kutokana na nguvu na spidi kutoka kwa wapinzani wao ambao walijua fika mabao mengi ndiyo yatakayowanusuru, na hivyo kujikuta wakiwaacha El-Merreikh wakitawala kwa kiasi kikubwa mchezo huo.
Dakika takribani 10 za mwisho kabla mchezo kumalizika hazitasahaulika kamwe kwa vijana hao wanaonolewa na kocha Joseph Omog, baada ya kuruhusu mabao mawili ya haraka.
Ndani ya dakika hizo, El-Merreikh walifanikiwa kupata bao la pili kutokana na uzembe wa safu ya ulinzi ya Azam na kuruhusu wapinzani wao kufunga.
Huku ikidhaniwa kwamba mechi hiyo ingeamuliwa kwa mikwaju ya penalty kutokana na ushindi wa bao 2-0 walioupata Azam kwenye mechi ya kwanza iliyopigwa katika Uwanja wa Azam Complex wiki mbili zilizopita, shambulizi la nguvu lililofanywa likaipatia El-Merreikh bao la tatu lililozima kabisa ndoto za Azam.
Kwa matokeo hayo, Azam imeyaaga mashindano hayo kwa kufungwa jumla ya mabao 3-2 na hivyo kuungana na wenzao wa Zanzibar, KMKM walioaga michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-1 licha ya ushindi waliopata mapema leo dhidi ya El Hilal.

No comments: