CUF YADAIWA KUKWAMISHA UCHIMBAJI MAFUTA ZANZIBAR


Wakati Wazanzibari wakisubiri mchakato wa kupiga kura  ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa kuruhusu kuanza uchimbaji mafuta na gesi, baadhi ya viongozi wakuu serikalini wameshutumiwa kupinga na kuhamasisha wafuasi kususa mchakato.

Makamu wa Kwanza wa Rais, Seif Sharif Hamad (pichani) ametajwa kuhusika na matamshi ambayo yanayoweza kukwamisha visiwa hivyo kuchimba nishati hiyo.
Ametajwa kutotabirika kimisimamo kutokana na kutoa kauli zinazokinzana anapokuwa chini ya wadhifa wake serikalini  wa makamu wa kwanza wa Rais na pale anapokuwa kwenye chama.
Imeelezwa kwamba, hivi karibuni  akiwa nchini Qatar ambako alikutana na  viongozi, wafanyabiashara na wawekezaji, aliwataka waje  kuwekeza akisema mazingira yameimarika kutokana na amani na utulivu.
Aidha, alisema Zanzibar iko katika hatua za mwisho za kukaribisha kampuni mbali mbali za nje kuwekeza katika mafuta na gesi; hatua inayosubiri kukamilika kwa mchakato wa kura ya maoni ya katiba itakayoruhusu Zanzibar kuchimba mafuta.
Seif alitoa kauli hizo katika nyakati tofauti wakati alipokutana na Waziri wa Nishati na Viwanda wa Qatar, Dk Mohamed Saleh Al-Sada. Asilimia 70 ya pato la taifa la nchi hiyo inatokana na gesi.
Hata hivyo, katika kile kilichoelezwa ni kubadilika ndani ya chama, katika hotuba yake  mwishoni mwa wiki wakati akizindua kamati za uchaguzi wa chama chake,  aliwataka Wazanzibari kususa mchakato wa kura ya maoni.
Alisema katika kuhakikisha kwamba huu ni mwaka wa uamuzi na siyo wa uchaguzi, aliwataka wananchi kususa mchakato wa kura ya maoni na kutaka wajipange kuhakikisha  CUF wanashinda katika uchaguzi mkuu na kushika dola.
“Wamepiga ngoma wenyewe, wamecheza wenyewe na sasa tuwaache wenyewe waicheze katiba hiyo ni ya Dodoma na ibaki huko huko,” alisema kwenye mkutano huo wa hadhara.
Kwa mujibu wa makamu huyo wa rais, Zanzibar haiwezi kupata maendeleo ya kweli kwa mfumo wa serikali mbili uliopo sasa  ambao ulipitishwa katika Katiba Inayopendekezwa.
"Mimi napinga Muungano wa Serikali mbili…kama tungekuwa na uwezo katika Muungano tuliokuwa nao sasa matukio ya kukataliwa kwa huduma za mashirika ya ndege kama Qatar na Uturuki kamwe yasingetokea,” alisema Seif.
Hata hivyo, kauli hizo alizotoa kwenye mkutano, zimepokewa kwa  hisia tofauti na wananchi wengi wa Zanzibar hususani wanaotaka mabadiliko wakiitaja kuwa ni ya kichochezi.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ali Vuai akizungumza na waandishi wa habari, alisema chama hakishangazwi na kauli alizoita za ‘ukigeugeu’ za kiongozi huyo wa CUF.
Vuai alisema mwaka 2010 wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CCM na CUF kwa pamoja walikubaliana na kufikia azimio la kutaka kuona mafuta na gesi yanaondolewa katika orodha ya mambo ya muungano.
Alisema la kushangaza ni kuona kwamba,  fursa waliyokuwa wanaitaka sasa imekuja ambayo itatoa nafasi ya Zanzibar kuchimba mafuta na gesi lakini  sasa wanapinga na kukataa moja kwa moja.
Alimtaja Seif kwamba,  yupo kuona kwamba kwa njia yoyote anaingia madarakani bila ya kujali maslahi ya Wazanzibari walio wengi.
"Mimi sishangazwi na kauli za Maalim Seif kwani akiwa Qatar alisema jambo jingine huku akihamasisha wawekezaji, lakini alipozungumza na wanachama wake ametoa kauli nyingine kabisa ya kutaka wafuasi wake na Wazanzibari kwa ujumla kususa mchakato huo,” alisema Vuai.
Akifafanua zaidi, alisema  Seif hataki kuona Muungano wa Tanganyika na Zanzibar udumu na kwamba ndiyo sababu anatoa visingizio kwamba wananchi wanauchukia.
Alitoa mfano kwamba, ajira nyingi za vijana zinazotoka Tanzania Bara ambapo vijana kutoka Zanzibar wamenufaika na ajira  Idara ya Uhamiaji na pia walimu wengi wamepata fursa kufanya kazi bara.
Kwa mujibu wa Vuai, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina uwezo wa kuwapatia vijana wengi kwa wakati mmoja ajira . Alihimiza vijana kutokubali kurubuniwa na kusikiliza kauli alizoita za upotoshaji zinazotolewa na Maalim Seif.
Wakati huo huo, baadhi ya wakazi visiwani hapa wameshauri Serikali kuimarisha ulinzi katika kipindi cha kura ya maoni kuepuka vurugu za wapinzani wanaoweza kuzuia wafuasi wa CCM kupiga kura.
“Tunaiomba Serikali kujitayarisha na kila aina ya fujo zitakazojitokeza katika kipindi cha mchakato wa kura ya amani kwani wapo wapinzani wameonesha nia ya kutishia kuharibu zoezi hilo,” alisema Ali Juma, mkazi  wa Mikunguni na kutaja hali hiyo kuanza kujitokeza Pemba.

No comments: