Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge Jumatano
atasimama mbele ya Baraza la Maadili kujibu tuhuma za kukiuka maadili ya
uongozi na kujipatia Sh bilioni 1.6 ambazo aligawiwa kutoka katika fedha za
akaunti ya Tegeta Escrow.
Profesa Anna Tibaijuka ambaye alitimuliwa
Uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi kutokana na kujipatia Sh bilioni 1.6 kutoka
kwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira atajibu tuhuma hizo
Alhamisi.
Ratiba iliyotolewa na Baraza la Maadili,
jijini Dar es Salaam inaonesha kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Katiba na Sheria, William Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, atasimama
mbele ya Baraza hilo Jumatatu ijayo.
Wengine
watakaopanda kizimbani ni Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma atakayehojiwa Jumatatu ijayo.
Wengine ni
Mnikulu Shaban Gurumo atakayehojiwa
Machi 4, akifuatiwa na Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip Saliboko na
Machi 6 atahojiwa Naibu Kamishna
Upelelezi na Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Loicy Appollo.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa Machi 9 atahojiwa
Mkurugenzi Mdhibiti Uchumi Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Dk
Benedict Diu akifuatiwa na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Gulam Remtullah.Akizungumza Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu Hamis
Msumi alisema ratiba ya kuwahoji viongozi, ilitakiwa kuanza jana ikianza na
aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho
Gambo. Hata hivyo, Gambo aliwasilisha barua kwamba anaumwa na atashindwa
kuhudhuria.Vievile,
Gambo aliwasilisha cheti cha daktari akitakiwa kupumzika kwa wiki mbili,
jambo lililosababisha Baraza hilo kuahirisha kusikiliza shauri lake hadi hapo litakapopanga kikao kingine.Kutokana na kuanza kuwapandisha kizimbani
watuhumiwa wa sakata la Escrow, Baraza
litatoa uamuzi wa ama wahusika hao wafikishwe mahakamani, au la, kulingana na
hatia watakazokutwa nazo.
Kashfa ya Escrow iliyonguruma mwaka jana
bungeni, imesababisha baadhi ya watuhumiwa kujiuzulu nyadhifa zao na wengine
kuvuliwa madaraka, akiwamo Profesa Tibaijuka aliyewekwa pembeni na Rais Jakaya
Kikwete Desemba mwaka jana.
Chenge alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Bajeti na aliachia wadhifa huo hivi karibuni. Ngeleja aliyekuwa Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Mbunge wa Lupa na Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini , Victor Mwambalaswa, nao walijiuzulu
hivi karibuni.
Chenge na Profesa Tibaijuka kila mmoja alipata
mgawo wa Sh bilioni 1.6 huku Ngeleja akipata Sh milioni 40.4 kutoka kwa James
Rugemalira wa VIP Engineering and Marketing Limited, zikiwani mgawo wa Tegeta
Escrow.
Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo
ya uwekezaji (capacity charges), zilizokuwa zinalipwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kabla
hazijakabidhiwa kwa anayelipwa, ambaye ni Kampuni binafsi ya kufua umeme ya
IPTL. Kabla ya hapo Tanesco ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa IPTL. Ilifunguliwa
ili kutoa nafasi kwa pande hizo mbili kumaliza tofauti zao kuhusu
kiwango cha tozo hiyo.
No comments:
Post a Comment