CCM YAKANA KUANDAA MGOMBEA UBUNGE ARUSHA


Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arusha, imesema chama hicho hakina mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, aliyeandaliwa hadi sasa.

Kimesema mgombea  mwenye sifa za kulikomboa jimbo hilo, ambalo liko Chadema, hajajitokeza mpaka sasa.
Akizungumza na mwandishi hivi karibuni, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Arusha ,Feruzi Banno alisema  chama kina utaratibu wake wa kampeni na chama hakina mgombea aliyeandaliwa kwa kuwa muda wa kuandaa wagombea bado haujatangazwa.
Banno alisema hayo alipotakiwa na gazeti hili, kufafanua kauli zilizozagaa jijini Arusha kuwa
chama hicho kimemwandaa mmoja wa wagombea (jina tunalo) ambaye yuko mstari wa mbele kulitaka jimbo hilo kwa udi na uvumba na tayari ameanza harakati za kampeni kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa CCM kata, wilaya na mkoa.
Alisema taarifa hizo zimekuwa zikisambazwa na wana CCM wenye kutaka ubunge Jimbo la Arusha, ambao wanaoana kama wanatengwa.
Alisema kura za maoni za kumsaka mgombea ubunge ndani ya chama, ndizo zitakazoamua na si vinginevyo na kamwe chama hakitambeba mwana CCM .
Pamoja na  hayo yote, Katibu huyo alisema Jimbo la Arusha lenye asilimia kuwa ya vijana, linahita mgombea mwenye kujichanganya katika rika zote na anayekubalika bila ya kubabaisha, kwani huyo atafanya chama kufanya kazi kwa urahisi na sio ngumu katika kampeni.
Banno alisema kuwa CCM inahamu ya kulikomboa Jimbo la Arusha Mjini hivyo hatuhitaji mgombea mzigo, ambaye itafika siku ya mwisho tukaanza kulaumiana hilo halitakubalika kamwe kwa uongozi wa chama wilaya.
‘’Tunataka mgombea kijana, mwenye kujichanganya katika vijiwe mbalimbali vya Jiji  la Arusha na mwenye kujulikana katika kila kona ya Jimbo la Arusha na mgombea huyo bado hajajitokeza hadharani. Hiyo itasaidia chama kufanya kazi ndogo sana lakina hatutaki mgombea ambaye chama kitafanya kazi ya ziada kumnadi, hilo halitakubalika kamwe. ‘’
Baadhi ya wana CCM waliojitokeza na kuonesha nia ya kuwania ubunge Jimbo la Arusha Mjini ni  Kamanda wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana  (UVCCM) Mkoa wa Arusha , Philemon Mollel na Wakili wa Kujitegemea, Victor Njau.
Mwingine ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana Taifa, Dk Arod Adamson na Deo Mtui.
Wengine wanaotajwa kuwania kiti hicho ni wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya wilaya ya Arusha,  mjumbe wa NEC Arusha, God Mwalusamba, Mweka Hazina wa Chama wilaya ya Arusha Victor Mollel, Katibu Mwenezi wa CCM wa wilaya ya Arusha, Gasper Kishimbua  na Halima Mamuya.
Baadhi ya wagombea hao tayari wengine wameshaanza kuchapisha fulana na kujitangaza kuwa ni wateuliwe wa chama, wenye lengo la kukomboa jimbo hilo la Arusha Mjini, hatua inayopingwa na chama ngazi ya Wilaya.

No comments: