BUNDUKI ILIYOPORWA NA ‘MAGAIDI’ TANGA YAPATIKANA



Polisi mkoani Tanga imesema imefanikiwa kupata bunduki aina ya SMG, ikiwa na risasi 20 ndani ya mapango ya Majimoto katika eneo la Amboni, inayodaiwa ilikuwa ikitumiwa na wahalifu waliorushiana risasi na askari  mwishoni mwa wiki.

Aidha, imesema inashikilia watu kadhaa akiwemo aliyesababisha kupatikana kwa bunduki hiyo.
Baadhi ya watu wanaendelea kuhojiwa, kupata taarifa kwa lengo la kukamata waliopora silaha kwa askari  na kurushiana risasi kwenye mapango hayo.
Kupatikana kwa silaha hiyo, kunafuatia msako maalumu uliodumu kwa siku nne sasa, uliolenga kusaka silaha na wahalifu wanaodaiwa kujificha ndani ya mapango ya mawe yaliyopo Amboni, nje kidogo ya mji wa Tanga.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja  alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari mjini hapa.
Alisema mafanikio hayo, yametokana na subira ya wakazi wa Tanga na ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuuonesha kwa Polisi inayoshirikiana na  vikosi vingine vya ulinzi na usalama, kufanya operesheni ya pamoja kwenye eneo hilo.
“Kutokana na taarifa kutoka kwa wananchi Februari 16 mwaka huu katika kitongoji cha la ‘Kona Z’ kilichopo Amboni, tulifanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye kwa sasa sitamtaja jina kwa sababu upelelezi unaendelea, tulimhoji kwa kina akatupa taarifa kuhusu silaha hii,” alisema.
Alieleza, “Tulikwenda mpaka pangoni na kufanikiwa kupata SMG hii ikiwa na magazini moja na risasi 20… silaha hii ni miongoni mwa zilizoporwa kwa askari mwezi uliopita”.
Alisema licha ya kupatikana kwa silaha hiyo, watu kadhaa wanashikiliwa wakihusishwa na tukio hilo.
Alisema upelelezi unaendelea kupata taarifa za kuwezesha kupatikana kwa silaha nyingine na vitu mbalimbali vilivyowahi kuibwa.
“Naomba wakazi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla muendelee kuvuta subira na kutoa ushirikiano…endelezeni utulivu na mshikamano kwa jeshi la polisi ili kwa pamoja tuweze kumaliza tatizo hili,” alisema.
Alisema upo umuhimu mkubwa kwa wananchi, kuendeleza utulivu kwa kutokubali kuamini taarifa potofu zenye kujenga hofu, zinazosambazwa na baadhi ya mitandao ya kijamii kwa kuwa zinalenga kuwavuruga.
“Kimsingi jeshi la polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama, linaamini na kuthamini kazi ya vyombo vya habari hasa vile makini, ambavyo vimeendelea kuwaarifu wananchi habari sahihi ambazo hazina ghilba wala kuwachanganya”, alisema.
Alikanusha taarifa zilizoenea mjini kwamba ipo miili ya wahalifu, iliyokutwa ndani ya mapango hayo, kutokana na mapigano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki.
“Ndugu zangu mwanzoni tulikuwa tukisikia harufu kali ya kama miili iliyooza, kweli tulijitahidi kutafuta na tukafanikiwa kuona mizoga ya ngedere na siyo binadamu ...wanyama hao walikuwa watatu na walikuwa na majeraha makubwa sana. Kwa hiyo hawakuwa watu, bali ni ngedere ndio walikokuwa wamekufa na kuoza humo pangoni,” alisema.
Akizungumzia mkakati wa kupata silaha iliyosalia na vifaa vingine vilivyoporwa, Chagonja alisema jeshi lake na kikosi cha operesheni hakitalala usingizi mpaka vitu vyote vipatikane.

No comments: