BABA MZAZI WA MTOTO ALBINO ALIYEUAWA GEITA ATIWA MBARONI


Mtoto Yohana Bahati mwenye ulemavu wa ngozi (albino), aliyetekwa katika Kijiji cha Ilelema wilayani Chato katika Mkoa wa Geita,  mwili wake umekutwa ukiwa umefukiwa huku umenyofolewa miguu na mikono.

Polisi imesema baba mzazi wa mtoto huyo, Bahati Misalaba na mkazi wa kitongoji cha Mapinduzi katika kijiji cha Lumasa, wilayani Chato, wamekamatwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Mwili wa mtoto huyo mwenye umri wa mwaka na miezi sita, ulikuwa umefukiwa katika moja ya mashamba ya mahindi  ndani ya hifadhi, huku pembeni yake kukiwa na kipande cha nguo kilichokuwa kimejaa damu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba mwili ulipatikana juzi saa 12 jioni.
''Mwili wa mtoto huyu ulipatikana ukiwa umefukiwa ndani ya kaburi dogo katika shamba la mahindi, mahali ambapo si makazi rasmi ya kuishi watu wakati jeshi la polisi kwa kushirikiana na raia wema walipokuwa katika harakati za kumtafuta baada ya kuwa ameibwa siku ya Jumapili saa 2.00 usiku akiwa amebebwa na mama yake,'' alisema Kamanda Konyo.
''Eneo jirani na lilipokuwa kaburi la mwili wa mtoto huyu kulikutwa kipande cha nguo chenye damu, lakini polisi walipofukua walikuta miguu yote na mikono ikiwa imenyofolewa, hali iliyotulazimu kuamini kuwa watekaji waliofanya ukatili huo watakuwa wameondoka na viungo hivyo,'' alisema.
Katika tukio hilo, watekaji  waliokuwa na silaha mbalimbali za jadi,  walimjeruhi  pia Ester Bahati (30), ambaye ni mama wa mtoto. Kwa sasa Ester  amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
''Msako tuliouendesha ulilenga kuokoa maisha ya mtoto huyu, lakini hatukuweza kufanikiwa katika hilo badala yake tumempata akiwa tayari amekwishafariki, hili ni tukio baya sana, lenye kuudhi lililojaa ukatili usioweza kuvumilika kwa mtu yeyote anayeamini katika Mungu,” alisema kamanda.
Aliahidi, “Tutaendelea kuwasaka wale wote waliohusika katika tukio hili, wakiwemo waganga wa jadi, naamini tutawakamata na siyo muda mrefu hakuna atakayebaki salama katika hili.''
Alitoa mwito kwa wananchi kutoruhusu tukio lingine la namna hiyo litokee, badala yake wachukue hatua mapema kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika vya dola viweze kudhibitiwa.
Alisema kila mtu anapaswa kutambua wajibu kuwa ulinzi na usalama ni suala la jamii nzima na siyo kuachia  polisi peke yake.
Aidha alitaka waandishi wa habari kusaidia kuibua matishio mbalimbali wanapokuwa wanatimiza majukumu yao hatua zichukuliwe.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kijijini, familia anayotoka mtoto huyo ina watoto wengine wawili wenye ulemavu wa ngozi ambao ni Tabu Bahati (3) na Shida Bahati  (12).
Wakati wa utekaji, watoto hao inaelezwa hawakuwa nyumbani hapo, bali walikuwa wakicheza nyumba ya jirani. Baba yao inadaiwa alikuwa nyumbani akiota moto.
Mama yao, Ester  anaendelea kutibiwa majeraha yaliyotokana na mapanga wakati akijaribu kumwokoa mtoto wake.
Hii ni mara ya pili ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili, tangu tukio kama hilo lijitokeze baada ya mtoto Pendo wa kijiji cha Ndami, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, kutekwa na watu wasiofahamika. Mtoto huyo hadi sasa hajapatikana.
Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini  na Mkurugenzi  Mkazi wa Shirika la Maendeleo la umoja huo (UNDP), Alvaro Rodriguez amehimiza serikali kuchukua hatua zaidi, kukabili mauaji ya watu wenye albinism.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuhusu kuuawa kwa mtoto Yohana, Mratibu huyo wa UN alisema pamoja na juhudi zilizopo sasa za kukabili mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu huo wa ngozi,  lazima ziongezwe.
Alisema katika kipindi cha miezi miwili, Tanzania imeshuhudia kutekwa nyara kwa watoto wawili katika Kanda ya Ziwa, akiwemo Pendo ambaye pamoja na juhudi za kumtafuta kuendelea, hadi sasa hajajulikani aliko.
Alisema Umoja wa Mataifa unasikitishwa na vitendo vya kikatili dhidi ya watoto hao wawili.
Mashambulio dhidi ya watu wenye albinism, yanaelezwa kuwa yanasababishwa na imani za kishirikina na kwamba kutoka mwaka 2000 hadi sasa,  watu 74 wenye ulemavu huo wameuawa.
“Mashambulizi haya yanaambatana na ukatili mkubwa, na wakati serikali inafanya kila juhudi kukabili tatizo hili, juhudi  kubwa zinastahili kufanywa ili kukomesha mauaji na  kulinda kundi hilo dogo la watu ambao wako katika hatari kubwa," ilisema sehemu ya taarifa hiyo. 
Alisema mashambulio dhidi ya albino, hayavumiliki, si halali kwa namna yoyote na yanaweza kukomeshwa. 
Mratibu huyo alipongeza juhudi za serikali katika kukabiliana na wimbi hilo la mauaji hayo.
Alisema Umoja wa Mataifa unataka mamlaka husika, kuhakikisha haki za raia zinalindwa na utawala wa sheria unazingatiwa.
“Tunataka mwaka 2015 kuwa mwaka wa haki za Watanzania wote zitaheshimiwa wakiwemo albino,” ilisisitiza. 
Mratibu huyo wa UN alisema amezungumza na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Fatma Mwassa na Chama cha Maalbino  ( TAS). Alisema alihakikishiwa kwamba wanafanya kila linalowezekana, kukomesha madhila dhidi ya maalbino.

No comments: