ASHITAKIWA KWA KUNAJISI MTOTO WA MIAKA MINNEMkazi wa Bangulo Hali ya Hewa, Baraka Benson (30) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, akikabiliwa na mashitaka ya kumnajisi mtoto wa miaka minne.

Benson alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassan Juma.
Wakili wa Serikali, Florida Wenslaus alidai kwamba Desemba 23 mwaka jana, maeneo ya Bangulo Hali ya Hewa Wilaya ya Ilala, Benson alimnajisi mtoto huyo wa miaka minne kwa kumtia vidole sehemu za siri huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande kwa kushindwa masharti ya dhamana.
Awali, wakili Wenslaus alidai kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshitakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Juma alimtaka mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambapo mmoja kutoka taasisi inayotambulika, watakaosaini dhamana ya Sh milioni mbili. Kesi itasikilizwa maelezo ya awali Machi 3 mwaka huu.
Katika tukio jingine, mkazi wa Ubungo, Sad Salimu (29) amepandishwa kizimbani katika mahakama ya mwanzo Kariakoo akikabiliwa na mashitaka ya wizi wa vifaa vya umeme jua.
Karani Lucy Rutabanzibwa alidai kwamba Desemba 16 mwaka jana, maeneo ya mtaa wa Msimbazi na Masasi, Salimu aliiba vifaa 57 vya umeme wa jua vyenye thamani ya Sh milioni 6.5 mali ya Kampuni ya Steps Entertainment.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande kwa kushindwa masharti ya dhamana. Alitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini kulipa Sh milioni 3.5. Kesi itatajwa Machi 2 mwaka huu.

No comments: