ANASWA AKIWA NA LUNDO LA VYETI FEKI


Mtu anayetuhumiwa kwa utapeli, amekamatwa wilayani Hanang’ mkoani Manyara akidaiwa kuwa na vyeti bandia vitatu vya ajira tofauti akidai ni mwalimu, ofisa mifugo na polisi.

Mtuhumiwa huyo, Hamis Yusufu alikamatwa katika kata ya Gissambalang’ wilayani Hanang kwa ushirikiano wa ofisi ya diwani pamoja na polisi jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Diwani wa kata ya Gissambalang’, Masala Bajuta, alisema mtu huyo alikamatwa  Januari 10 mwaka huu saa 11 kwenye shule ya sekondari Gissambalang’.
Alikamatwa  baada ya walimu kumtilia shaka akidai anafanya mazoezi kwa vitendo shuleni hapo.
Kwa mujibu wa diwani, mtu huyo alifika shuleni hapo na kupewa hifadhi na mmoja wa walimu baada ya kujitambulisha kwamba amefika kufanya mazoezi kwa vitendo. Alipotakiwa kuonesha  vitambulisho na vyeti vyake, alidai kuwa alivisahau mjini Katesh.
“Huyu mtu Hamis Yusufu alikuwa haeleweki mara aseme yeye ni mwalimu, mara yeye ni askari polisi wa upelelezi, mara yeye ni ofisa mifugo na alipobanwa zaidi alidai kuwa yeye ni mwananchi wa kawaida tu,” alisema Bajuta.
Alisema Polisi Jamii walipompekua walimkuta na vyeti vitatu vilivyopigwa mihuri japokuwa vingine havikuwa na picha yake. Alisema  kitambulisho kimoja kilikuwa na  picha ya Ofisa Mifugo, George Lwakatare ikionesha ameajiriwa mjini Singida.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Christopher Fuime
alithibitisha kukamatwa kwa mtu huyo na kusema anashikiliwa kwenye kituo cha Polisi Katesh wilayani Hanang’ kwa uchunguzi zaidi.
“Tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na pindi utakapokamilika tutamfikisha mtuhumiwa huyu mahakamani kwa kosa la kughushi vyeti na kudanganya kuwa yeye ni mtumishi wa serikali ili hali siyo kweli,” alisema Kamanda Fuime.

No comments: