Wanasiasa
wamenyooshewa vidole, wakihusishwa na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi
baada ya matukio hayo kuhusishwa na harakati za kuelekea katika uchaguzi mkuu.
Vyama
vya watu wenye ulemavu pamoja na baadhi ya wadau kutoka vyama vya siasa,
vimetaka Serikali kutopuuzia dhana hiyo ya kuhusisha harakati za kisiasa na
mauaji hayo.
Aidha, Chama cha Walemavu wa Ngozi Tanzania,
kimesema kiko katika maandalizi ya kufanya maandamano ya amani hadi Ikulu kwa ajili
ya kumwona Rais Jakaya Kikwete wapange mikakati ya kutokomeza mauaji hayo ya ukatili .
Akizungumza
katika mkutano ulioandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Walemavu na Vyama vya
Siasa nchini, mwanachama kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Abdallah
alisema katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi, alisema albino wanaishi
kwa wasiwasi kutokana na uwezekano wa mauaji hayo kuanza kuibuka tena kwa kasi.
“Mimi
mwenyewe nina tatizo la ngozi (albino), hivi sasa tuko kwenye kipindi cha
uchaguzi, na tetesi ni kwamba wengi wanauawa kwa imani potofu za baadhi ya watu
kutaka madaraka, tusaidieni jamani ukweli ni kwamba tunaishi kwa hofu,”
alisema.
Alisema
ni vyema Serikali ikaacha kupuuzia tetesi hizo za kuwahusisha baadhi ya watu
wanaotaka madaraka na kuagiza watu wenye ulemavu wauawe kwa imani za
kishirikina.
Alitaka
hatua madhubuti zichukuliwe kuokoa maisha ya Watanzania hao.
“Jamani
tujue kuwa hii ni damu inayomwagika ni ya ndugu zetu, kama hatua
zisipochukuliwa inaweza kuwa laana kwa vizazi vyetu. Tukijipanga Tanzania
tunaweza kuwa salama,” alisisitiza.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wakulima (AFP), Said Soud
alisema jamii inatakiwa kutambua kuwa ni dhambi watu kufikiria kuwa wanaweza
kupata utajiri na madaraka kupitia mauaji au viungo vya watu wenye ulemavu.
“Hili
naomba likemewe kwa nguvu zote, hii ni dhambi kubwa, sisi wanasiasa tutumie
majukwaa kukemea dhambi hii, lakini pia Serikali nayo itekeleze kwa vitendo
sheria zilizopo na kuwaadhibu vikali wale wote wanaohusika na dhambi hii,”
alisema.
Mwenyekiti
wa Chama cha Walemavu wa Ngozi Tanzania, Ernest Kimaya kwa upande wake alisema,
kwa sasa tatizo hilo linazidi kuwa sugu.
Alisema
tangu mauaji hayo yaanze mwaka 2006, hadi juzi alipouawa Yohana Bahati,
maalbino 76 wameuawa kikatili na watu wasiojulikana.
Ushirikina
Hivi
karibuni, katika semina iliyoandaliwa na Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania
(ALAT), baadhi ya washiriki walitaja uchaguzi mkuu kuchochea ongezeko la mauaji
ya wenye ulemavu kutokana na wagombea kutumia mbinu chafu na dhaifu.
Katika
semina hiyo iliyofadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika lake la
Kimataifa la Maendeleo na Misaada (Sida), ilielezwa na baadhi ya wachangiaji
kwamba, ongezeko la mauaji ya albino katika kipindi cha uchaguzi, linatokana na imani potofu miongoni mwa
wanasiasa uchwara.
Miongoni
mwa wachangiaji katika semina hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Diwani wa
Kata ya Sunya, wilayani Kiteto, Manyara, Mussa Brighton (CCM) aliyeomba
serikali kutafuta mbinu za kudumu za kukabili wanasiasa wa aina hiyo.
Juzi,
Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja huo
(UNDP), Alvaro Rodriguez katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, pia
aligusia kuwapo taarifa zinazohusisha wanasiasa na mauaji hayo.
Alisema
mashambulio dhidi ya watu wenye albinism, yanaelezwa kuwa yanasababishwa na
imani za kishirikina na kwamba kutoka mwaka 2000 hadi sasa, watu 74 wenye ulemavu huo wameuawa.
Maandamano
“Kutokana
na tatizo hili kuzidi kuwa sugu chama chetu kimeanza maandalizi ya maandamano
ya amani na kupeleka kilio chetu kwa Rais ili tuweze kushauriana utaratibu wa
kupata suluhu ya kudumu ya tatizo hili,” alisema Kimaya.
Alisema
katika maandamano hayo watayafanya Machi 2, mwaka huu na kwamba, pamoja na
kupeleka kilio hicho kwa Rais, pia watafanya sala maalumu kwa ajili ya wote waliopoteza maisha yao kwa kuuawa
kikatili.
No comments:
Post a Comment