ALAMA UFAULU ZATESA WAMILIKI SHULE BINAFSI


Siku chache baada ya Serikali kusema itazifutia usajili shule zitakazokaidi agizo la kuweka viwango maalumu na tofauti vya ufaulu kutoka kidato kimoja kwenda kingine, wadau wa elimu wamezungumza na kusema agizo hilo linalenga kuua ubora wa taaluma nchini.

Akizungumza na mwandishi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Benjamin Mkoya alisema viwango vinavyowekwa na shule binafsi vinakubaliwa na wazazi na kuwa kinyume chake shule hizo zitakufa kutokana na uwezekano wa kufifia ubora wa kitaaluma.
“Viwango vinavyoweka huwa vinakubaliwa na wazazi, na lengo la kufanya hivyo ni kutaka shule zifanye vizuri hivyo kuweza kujiendesha, kwani mbali na kutoa huduma, tunafanya biashara,” alisema Mkoya.
Alisema suala la baadhi ya shule kupanga viwango vya ufaulu limekuwa likifanyika muda mrefu na kuridhiwa na wizara husika ya elimu Julai 2013, baada ya agizo la kuifungia shule ya sekondari ya Mwilavya, Kasulu mkoani Kigoma iliyopandisha viwango vya ufaulu hadi kufikia asilimia 45 kutokana na matakwa ya wazazi.
Mkoya alisema suala hilo lilifika wizarani na uongozi wa TAMONGSCO kukutana na Naibu Waziri (wakati huo akiwa ni Philipo Mulugo) ambaye alisema kama wazazi wameridhia viwango hivyo, shule zinatakiwa kuendelea kufuata viwango hivyo.
“Tulikutana na uongozi wa wizara, na hapa hatumuangalii mtu aliyekuwepo ofisini bali taasisi,” na tulizungumza hilo, na hapo walisema kama wazazi wanaridhia viwango hivyo basi hakuna sababu ya kugombana na wapiga kura ambao wanataka viwango vya juu,” alisema na kuongeza kuwa kwa mwaka huu pekee wameshafanya vikao na viongozi wa Wizara ya Elimu mara mbili kwa lengo la kuboresha sera ya elimu na suala zima la Matokeo Makubwa Sasa (BRB).
Aidha, Mkoya alisema Serikali imekuwa ikitoa maagizo mbalimbali yanaonekana kulenga kudhoofisha shule zisizo za serikali, na  kutolea mfano wa agizo lililotangulia lililotolewa na TAMISEMI likizitaka shule hizo kutosajili wanafunzi mpaka hapo shule za serikali zitakapojaa.
“Serikali inatakiwa kutoona shule hizi kama ni ebola na kuzipiga vita, badala yake wazione kama partner (mshirika) katika kuboresha elimu hasa katika kufikia BRN.
Mkoya alisema wakati umefika sasa, sekta ya elimu kuwa na taasisi huru ambayo itasimamia elimu hapa nchini hivyo kuondoa mgongano wa kimaslahi kutoka kwa serikali ambayo ni wamiliki wa shule na pia ndio wanaosimamia elimu.
“Tunataka mamlaka huru kama ilivyo SUMATRA, Wizara ndio yenye shule na ndio inayosimamia elimu, hapa hapatakuwa na usawa,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Huduma ya Elimu kwa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) ambayo ni Bodi ya muungano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo (CCT),  Petro Pamba alisema shule zao hazitakwepa  mfumo wa kupanga viwango vya ufaulu kwani unaandaa wanafunzi na uwajibikaji kwa walimu.
Alisema taasisi yake yenye shule za sekondari 368 nchi zima imekuwa ikiendesha shule kwa mifumo miwili ambayo ni shule za seminari ambayo zinalenga kuwaandaa watumishi wa kanisa na ile ya kutoa huduma ya elimu kwa jamii.
Alisema mfumo wa kupanga viwango vya ufaulu umekuwa ukitumika muda mrefu na kujulikana na wizara na kwa sasa hawawezi kuukwepa kwani umekuwa ukiwaandaa vizuri wanafunzi na uwajibikaji kwa walimu.
“Mfumo wa kuweka viwango vya ufaulu unawafanya walimu pia wajitathmini, ukiwaacha walimu huru basi nao wanabweteka, hivyo sisi tutaendelea na mfumo huo kwani umekuwa ukifanyika muda mrefu na mamlaka za elimu zinaelewa,” alisema.
Alisema viwango vilivyopo sasa ni kati ya asilimia 40 hadi 49 na kuwa zaidi ya asilimia 50 kwa shule za seminari ambazo zinaandaa watumishi wa kanisa.
“Huko kwenye seminari mchujo wetu ni mkali sana kwa sababu ndio tunaowaandaa watumishi ambao watakuwa wakihudumia jamii hivyo kutakiwa wawe vizuri kichwani,” alisema.
Hata hivyo, Pamba alisema taasisi yao inakamilisha mfumo mbadala wa kuwasaidia wanafunzi wanaoelewa taratibu kwa kuwaandalia mafunzo maalumu ili waweze kufanya vizuri mitihani ya mwisho na kuwa wale wenye alama za chini watalazimika kurudia darasa.
Alisema pamoja na Wizara kutaka shule kufuata Sera ya Elimu inayotaka viwango vya ufaulu kuwa ni asilimia 30,  alisema sera hiyo inaelekeza kwa wanafunzi wanapotakiwa kuvuka kutoka kidato cha pili kwenda cha tatu na si katika madarasa mengine.
Alisema pia kiwango hicho cha ufaulu ni cha chini ukilinganisha na mfumo mpya wa upangaji wa alama za ufaulu unaofanywa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ambayo ufaulu ni kati ya alama 40 hadi 49 (C), huku alama 30 hadi 39 ni ufaulu hafifu ambao unatoa daraja D.
Alisema kutokana na alama hizo kupitwa na wakati, CSSC, imepeleka pendekezo wizarani kutaka kubadilishwa kwa viwango vya ufaulu hadi kufikia alama 40 kwa kidato cha pili kwenda cha tatu.
Alipoulizwa Katibu wa Elimu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mohammed Jongo alisema: ”Wizara ndio wasajili wa shule hapa nchini hivyo tutatekeleza agizo lao.”
Kwa nyakati tofauti wakijibu maswali bungeni, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu wake Anne Kilango Malecela walisema serikali itazifutia usajili shule zote za serikali au binafsi, zitakazobainika kukaidi agizo la kuacha kuweka viwango maalumu na tofauti za ufaulu kutoka kidato kimoja kwenda kingine.
Waraka wa Elimu Namba 6 wa mwaka 2011, umetoa maelekezo kuhusu wastani wa ufaulu katika mtihani wa kidato cha pili ambapo kiwango cha alama ya ufaulu ni asilimia 30 tu na si vinginevyo kwa shule za serikali na binafsi.

No comments: