Ajira 40,735 zimezalishwa ndani ya miezi
mitatu kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana na kufanya jumla ya ajira 173,787
kupatikana kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana.
Wizara ya Kazi na Ajira imesema ongezeko hilo
la ajira limejitokeza katika maeneo makuu mawili ikiwemo ajira serikalini
ambazo ni 2,652 sawa na asilimia 6.5 na ajira kupitia sekta rasmi binafsi
ambazo ni 38,083 sawa na asilimia 93.5.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam, Msemaji wa Wizara hiyo, Ridhiwan Wema alisema takwimu hizo
zinaonesha kwamba sekta binafsi imeendelea kuwa mhimili wa uzalishaji wa ajira
nchini kutokana na serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya waajiri
kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.
“Katika kipindi cha nusu mwaka sekta binafsi rasmi ambayo ndiyo mwajiri mkuu
ilizalisha ajira 173,787 kupitia uwekezaji binafsi ambapo uwekezaji kupitia
ujenzi zilizalishwa ajira 107,527, uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) ajira 34,184 na
Sekta ya Mawasiliano ajira 342” alisema.
Alisema hatua zinazochukuliwa kwa sasa ni
pamoja na kufanya marekebisho ya Sera ya Ajira ya 2008, Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini Namba 6,2004, Sheria ya Taasisi za Kazi namba 7,2004 pamoja na
kutunga sheria Mpya ya Ajira za Wageni ambayo imelenga kulinda ajira za
Watanzania, kuboresha mazingira ya biashara na kuhamasisha uwekezaji.
Alishukuru wadau mbalimbali kwa ushirikiano
wao kwa kutoa taarifa za ajira kwa wakati. Alitoa mwito kwa waajiri wote nchini
kutoa ushirikiano katika ukusanyaji taarifa za soko la ajira.
“Taarifa hizi zimelenga kuiwezesha serikali
kujua hali ya ajira nchini na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na
kuwezesha serikali kupanga matumizi sahihi ya nguvu kazi nchini,” alisema.
Alisema taarifa hizo ni miongoni mwa vigezo
vikuu vinavyotoa picha halisi ya mafanikio ya kiuchumi na kimaendeleo kwa nchi
au mahali husika na zinasaidia kupanga, kutekeleza na kupima ufanisi wa mipango
ya kiuchumi nchini pamoja na kupima uwezo wa kiuchumi katika wakati husika.
No comments:
Post a Comment