Mkazi wa kijiji cha Makutupa kata ya Lupeta wilaya ya
Mpwapwa mkoani Dodoma, Yusuph Chatambala (45) amehukumiwa kifungo cha maisha
gerezani baada ya kukiri kumnajisi mtoto mwenye umri wa miaka minne.
Ilidaiwa mahakamani kwamba mwanamume huyo alimpatia mtoto huyo
wa kike Sh 500 asitoe siri baada ya
kumnajisi, Februari 20, mwaka huu.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mwanamume huyo alitenda kosa
hilo baada ya kumkamata mtoto huyo akicheza na watoto wenzake jirani na
nyumbani kwao, kisha kumpeleka kwenye shamba la mahindi na kumnajisi.
Hukumu dhidi ya mshitakiwa huyo, ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa, Pascal
Mayumba baada ya kumtia hatiani mshtakiwa kutokana na kukiri mashitaka.
Akisoma hukumu, Hakimu alisema siku ya tukio, Chatambala
baada ya kumaliza alimpatia mtoto huyo Sh 500 na kuondoka zake huku akiwa
amemjeruhi mtoto huyo sehemu za siri .
Alisema kutokana na
mshtakiwa kukiri kosa, kwa mujibu wa sheria,
mtu yeyote anayefanya kosa la kumbaka mtoto chini ya miaka 10 anastahili
kifungo cha maisha jela.
Alipopewa nafasi ya kujitetea kabla ya hukumu, mshtakiwa
alikiri kufanya kitendo hicho. “Kweli mheshimiwa mimi nakiri kutenda kosa hilo
hivyo naomba Mahakama yako inisamehe tu sitarudia tena,” alidai.
Mwendesha Mashitaka
wa Polisi, Godwin Ikema aliomba Mahakama itoe adhabu kali iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hiyo.
Hakimu Mayumba alisema
kutokana na kosa kuwa la kikatili
na kwa kuzingatia sheria,
Mahakama inampa adhabu ya
kutumikia kifungo cha maisha gerezani.
Alisema kwa mtu yeyote ambaye hajaridhika na adhabu hiyo,
ana haki ya kukata rufaa ndani ya siku
30. Hakimu alipokuwa akitoa hukumu hiyo
mahakamani, mshitakiwa huyo alikuwa akitokwa machozi.
Kwa
mujibu wa hati ya mashitaka, alimfanyia kitendo hicho Februari 20 mwaka huu saa
12:00 jioni katika kijiji cha Makutupa.
No comments:
Post a Comment