WATANO WAFA AJALINI WAKIMPELEKA MJAMZITO HOSPITALI

Watu watano wakiwamo watatu wa familia moja wamekufa na wanne kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei alisema kuwa watu hao walikuwa wakimpeleka mgonjwa hospitali. Kamanda Matei (pichani) alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 5 mwaka huu majira ya saa 6:30 mchana huko eneo la Fukayosi Tarafa ya Msata wilaya ya Bagamoyo. 
Alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha gari namba T 252 DCB aina ya Toyota Noah lililokuwa likiendeshwa na Ramadhan Masapala (32) lililokuwa likitokea kwenye kituo cha afya cha Miono kuelekea hospitali ya wilaya ya Bagamoyo. 
“Gari hilo lilipasuka tairi la nyuma na kuacha njia kisha kuanguka bondeni na kusababisha vifo hivyo na majeruhi hao,” alisema Matei.
Aidha, aliwataja watu waliokufa ni pamoja na dereva Masapala, Mnamisima Semhoro, Stamili Semhoro na Nemganga Semhoro wote wakazi na wakulima wa Miono. 
Aliwataja majeruhi wa ajali hiyo ni pamoja na mjamzito aliyekuwa akipelekwa hospitali, Shukuru Jaba (30) na muuguzi wa kituo cha afya cha Miono, Mariamu Omary.
 Kamanda Matei alisema miili ya marehemu hao ilipelekwa hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo huku majeruhi wawili wakipelekwa kituo cha afya cha Miono huku mama mjamzito akiandaliwa kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

No comments: