WABUNGE WANAWAKE 19 WA TANZANIA KUZURU CHINA


Wabunge wanawake 19 wa Bunge la Tanzania wako China katika ziara ya siku 11 yenye lengo la kubadilishana na kujifunza kwa wenzao masuala ya uongozi na wanavyojihusisha kwenye shughuli za kijamii.

Akizungumzia ziara hiyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge  Wanawake wa Bunge la Tanzania, Anna Abdallah alisema moja ya malengo ya ziara yao wabunge hao  ni kujifunza jinsi ya kuwajumuisha wanawake kwenye uongozi.
"Mwaka huu ni wa uchaguzi na lazima tuwaandae watakaogombea nafasi za uongozi, kwa hiyo hii ni ziara ya mafunzo ya uongozi na kuangalia maendeleo, nia yetu kubwa ni kuona wenzetu jinsi wanavyowasaidia wanawake kuondokana na umaskini," alisema.
Bunge la Tanzania lina asilimia 20 ya wabunge wanawake na kwenye uchaguzi ujao huenda idadi ya wanawake ikaongezeka.
Makamu Mwenyekiti, Susan Limo alisema, "Licha ya Beijing tutaenda Ghuanzhou, pia tutakutana na kundi la wabunge wanawake wa China na naibu waziri anayeshughulikia masuala ya wanawake."
Anasema pia wakiwa hapa China, watajadili masuala ya kuendeleza uchumi wa Tanzania kama vile sekta ya utalii na biashara.
Ziara hiyo ya wabunge wa Tanzania nchini China ni sehemu ya mpango wa mabadilishano kati ya mabunge ya nchi hizo mbili.
Balozi wa Tanzania nchini China, Abdulrahman Shimbo alisema, "tunategemea kwamba watakuza uhusiano haya na kwamba wataweza kushirikiana katoka baadhi ya maeneo ya maendeleo na tunategemea zaidi hasa kuwasaidia wanawake kwa upande wa elimu."

No comments: